Friday, April 29, 2016 .Kuachiwa Huru Abdallah Zombe na Wenzake kusikilizwa Leo
Friday, April 29, 2016
Mahakama ya Rufaa leo inatarajiwa kusikiliza rufaa ya kupinga kuachiwa huru
kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO) Kamishna
Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na askari wenzake wanane waliokuwa
wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa
na Jaji Bernard Luanda, wengine ni Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles
Kaijage.
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alikata rufaa mwaka 2013, akipinga hukumu
ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyowaachia huru Zombe na
wenzake, baada ya kuwaona hawana hatia katika kesi ya mauaji ya watu
wanne iliyokuwa inawakabili.
Katika rufaa hiyo, DPP anadai kuwa Jaji Salum Massati alikosea kuwaachia
huru washitakiwa hao kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia
hatiani wote.
Mbali na Zombe, wajibu rufaa wengine ni ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed
Makelle, Konstebo Jane Andrew, Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael
Shonza, Koplo Abeneth Salo, Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Katika kesi ya msingi inadaiwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo
Mbezi Luis, Dar es Salaam Zombe na wenzake waliwaua kwa makusudi
wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias Lunkombe,
Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, pamoja na dereva teksi
Juma Ndugu.
Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Agosti 17, 2009, Jaji Massati aliwaachia huru
washitakiwa kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha mashitaka
dhidi yao bila kuacha shaka na Mahakama ikiwaona hawana hatia kwa makosa
yaliyokuwa yanawakabili.
Oktoba 6, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu hiyo
kwa madai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, pia
kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira unaotosha kuwatia hatiani
washtakiwa wote.
Hata hivyo Mei 8, 2013 Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa hiyo kutokana
na dosari za kisheria zilizobainika kwenye rufaa, lakini DPP alipeleka maombi
Mahakama Kuu ili aruhusiwe kukata tena rufaa nje ya muda.
Mahamaka Kuu ilikubali maombi yake, akakata tena rufaa inayotarajiwa
kusikilizwa leo.
No comments