BASATA KUADHIMISHA SIKU YA MUZIKI WA JAZZ
Saturday, 30 April 2016
National Arts Council BASATA
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushirikiana na Shirika la
Umoja wa Mataifa linalojishughulisha na Elimu na Sayansi
(UNESCO) litaungana na wasanii mbalimbali nchini na wadau wa
Sanaa kuazimisha siku ya muziki wa Jazz duniani ambayo kwa
mara ya kwanza itaazimishwa nchini Mei 2, 2016.
Maazimisho hayo ambayo yatapambwa na burudani mbalimbali
kutoka kwa Wasanii wa muziki wa jazz hususan Band maarufu ya
Das Jazz yanatarajiwa kufanyika kwenye Ukumbi wa Baraza hilo
ulioko Ofisi za BASATA Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam.
Sambamba na burudani hizo, kutakuwa na mada mbalimbali
zitakazowasilishwa na wadau wa muziki huu wa jazz ambazo
zitalenga kuamsha ari, thamani na ufahamu wa muziki huu
maarufu duniani miongoni mwa wasanii nchini.
Wawasilishaji wa mada hizo pamoja na mada zao kwenye mabano
ni pamoja na John Kitime (Matumizi ya neno Jazz), Carola Kinasha
(Uhusiano kati ya Elimu ya Muziki na Jazz) na Kurwigira Mareges
(Historia ya Muziki wa Jazz) na Masoud Masoud (Ujue Muziki wa
Jazz)
Mbali na burudani na mada hizo kuhusu muziki huo wa Jazz
kutakuwa na wageni waalikwa kutoka kwenye balozi na vituo vya
Utamaduni vya nchi mbalimbali zilizopo hapa Tanzania
BASATA linatoa wito kwa wasanii na wadau wa muziki huu wa
jazz kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho haya ambayo
yatakuwa yakifanyika kila mwaka sambamba na mataifa mengine
duniani.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
Katibu Mtendaji – BASATA
No comments