Thursday, April 28, 2016 Madiwani wa Chadema Wilayani Hai Wasusa Kuhudhuria Kikao cha Mkuu wa Mkoa Said Meck Sadiki


Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai wakiongozwa na Mwenyekiti wa
Halmashauri hiyo, Helga Mchomvu, wamesusa kuhudhuria kikao cha Mkuu wa
Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki wakati akizungumza na viongozi wa
vitongoji, vijiji, kata, viongozi wa taasisi za serikali na dini.
Sadiki alifika wilayani Hai jana, ikiwa ni moja ya ziara zake katika wilaya zote
za Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kuzungumza na
viongozi mbalimbali wanaowakilisha wananchi, pamoja na kusikiliza kero
zinazozikabili wilaya hizo.
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri,
Usharika wa Hai Mjini, madiwani hao ambao wote ni wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hawakuonekana hata mmoja huku eneo
walilokuwa wameandaliwa likibaki na viti vilivyo wazi.
Awali, Mkuu wa Mkoa alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa lengo la
kupokea taarifa ya wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mchomvu aliwasili kwa
kuchelewa na muda ulipofika wa kuelekea ukumbini, alitokomea kusikojulikana.
Hali hiyo ilimshangaza Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa ambaye
alisema siasa ziliisha baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana,
lakini inashangaza kwenye masuala ya maendeleo ya wananchi bado viongozi
wanaendelea kuziendekeza.
Byakanwa alisema, licha ya madiwani wote 17 wanaounda Baraza la Madiwani
Wilaya ya Hai kuwa ni wa Chadema, bado wanasimamia na kutekeleza Ilani ya
Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichopewa ridhaa na
Watanzania kuongoza kwa awamu nyingine ya tano.
“Ni jambo la kushangaza kuona viongozi waliochaguliwa na wananchi
wanashindwa kuwakilisha wananchi wao katika kupeleka na kuzisemea kero zao
mbalimbali zinazowakabili, na badala yake wamekuwa wakisusa vikao vya
kupanga maendeleo. Kwa siasa hizi wananchi hawawezi kupata maendeleo,”
alisema Byakanwa.
Akiwasilisha taarifa za kutofika kwa madiwani hao, Katibu wa Mbunge wa
Jimbo la Hai, Rosemary Kuringe alisema, amewasiliana na madiwani wake na
kuelezwa kuwa hawakupata taarifa za ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa.
Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na viongozi mbalimbali, Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Saidi Mderu alikiri kutoa taarifa
kwa madiwani wote katika kikao cha Baraza Maalumu la Madiwani
kilichofanyika Aprili 22, mwaka huu.
“Kwa suala hili la viongozi hawa kususa, namwachia Mungu, niliwapa taarifa
madiwani wote tena nilisisitiza, cha kushangaza wakati Mkuu wa Mkoa
amewasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mwenyekiti wa Halmashauri alifika
akiwa amechelewa lakini wakati tumekuja kwenye ukumbi hatukumuona,”
alisema Mderu.

No comments