Thursday, April 28, 2016 Wabunge Mabubu kubanwa Bungeni ,Ni wale wanaoshiriki Vikao vya Bunge Lakini Hawachangii Chochote


Kiti cha Spika wa Bunge kimesema ipo haja ya kufanya marekebisho ya Sheria
pamoja na Kanuni ili kila mbunge apate posho kulingana na kazi aliyofanya
bungeni, badala ya utaratibu wa sasa wa kuangalia mahudhurio pekee.
Aidha, kimewataka wabunge kubadilika na kuacha tabia ya kuchukua posho za
vikao vya Bunge bila kuzitolea jasho.
Kauli hiyo imekuja kutokana na Mwongozo ulioombwa Aprili 25, mwaka huu na
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) ambaye alikitaka kiti cha Spika
kutoa Mwongozo kuhusu usahihi wa wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kulipwa posho na mishahara wakati hawashiriki na kutimiza wajibu
wao wa kuchangia kwenye mjadala wa Bunge la Bajeti linaloendelea katika
Mkutano wa Tatu wa Bunge la 11.
Bashe alisema mbunge huyo alitumia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni za Kudumu za
Bunge akiomba Mwongozo wa Spika kutokana na Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni, kuamua kutoshiriki mjadala unaoendelea bungeni, lakini wabunge hao
wanasaini na kulipwa mishahara na posho.
Hivyo akaomba Mwongozo endapo ni haki kwa wabunge hao kupokea posho
wakati hawashiriki wala kutimiza wajibu wao wa kisheria.
Katika kujenga hoja hiyo, Bashe alitumia Ibara ya 63(3) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania isemayo, “Kwa madhumuni ya utekelezaji wa
madaraka yake Bunge laweza kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa
Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa bajeti.”
Aidha, Bashe alitumia Ibara ya 73 ya Katiba ya Tanzania kufafanua kuhusu
malipo ya mshahara, posho na malipo mengine kwa wabunge.
Akitoa Mwongozo wa Spika, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema
kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, Ibara ya 73 imeainisha masharti ya kazi ya
wabunge.
Alisema mbunge anastahili kulipwa mshahara kwa kila mwezi, na kufafanua
kuwa mbunge anapohudhuria vikao bungeni na kamati atalipwa posho ya vikao
kwa kiwango kitakachowekwa na Serikali na Kanuni za Bunge.
Alisema malipo ya mshahara ni suala la Kikatiba na Sheria hulipwa kwa mbunge
kutokana na kazi yake ya ubunge.
Hivyo malipo ya posho kwa wabunge yanatokana na mahudhurio yao bungeni
na siyo kwa kuchangia kama ambavyo wengi wao wanapenda iwe hivyo.
“Kimsingi kuhudhuria bungeni pekee siyo njia inayopendeza kwa kuwa mbunge
anapofika bungeni anatarajiwa atekeleze majukumu yake yalivyoainishwa katika
Ibara ya 63.
“…Tabia hii ya kutochangia mijadala na kuzunguka zunguka bungeni haikubaliki
na haitakiwi kuendelea, kila mbunge atekeleze wajibu wake na sio anahudhuria
ili alipwe posho,” alisema Dk Ackson.
Wakati huo huo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko katika
Kamati mbalimbali za Bunge, kwa kubadilisha wabunge 16 wa Kamati za Awali
kwenda nyingine.
Aidha, Spika amewapangia Kamati wabunge wapya wanne, walioapishwa
mwanzoni mwa Mkutano huu wa Bunge, ambao ni Shamsi Vuai Nahodha, Rita
Kabati, Oliver Semuguruka na Lucy Owenya.

No comments