Monday 25 April 2016 Matukio Ya Ubakaji Yaongezeka Nchini Na Kufikia 1765.


Matukio ya ubakaji hasa kwa watoto wadogo yamekuwa yakiongezeka kwa
kiwango kikubwa, ongezeko hili limebainika kutokana na ufuatiliaji tulioufanya
kupitia matukio yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi ambapo katika kipindi cha
mwezi Januari hadi Machi 2016 kumeripotiwa matukio 1765 ukilinganisha na
matukio 1585 katika kipindi kama hicho mwaka 2015 ikiwa ni ongezeko la
matukio 180.

Katika matukio ya Januari hadi machi 2016, jumla ya watuhumiwa 823
wamekamatwa na kufikishwa mahakamani ingawa bado kumekuwa na tabia ya
wazazi na walezi kuficha watuhumiwa wa ubakaji na kumaliza kesi hizo kirafiki
au kifamilia jambo ambalo ni kinyume cha sheria bila kuzingatia madhara
aliyoyapata mtoto.

Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linakemea vikali wale wote
wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu vya ubakaji na wazazi ama walezi
wanaofumbia macho vitendo hivyo na kuingia makubalino na watuhumiwa kwa
kupeana fedha kama fidia ili wamalize kesi kiundugu au kifamilia.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa Wazazi, walezi, Viongozi wa dini, Asasi za
kiraia, walimu na Wananchi kwa ujumla kuendelea kutoa ushirikiano katika
kushughulikia vitendo hivyo ikiwemo kuwafichua wazazi au walezi wanaofanya
makubaliano ya kumaliza kesi za ubakaji kirafiki au kifamilia ili kukomesha
vitendo hivyo.

Imetolewa na:
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.

No comments