Friday, April 29, 2016. Serikali Yashauriwa Kuwa na Hisa Kwenye Kampuni za Madini ili Kujua Mapato halide Yanayoingizwa na Wawekezaji wa Kigeni


Serikali imeshauriwa kuwa na sehemu ya umiliki katika kampuni zinazochimba
madini na gesi ili kujua mapato halisi yanayoingizwa na wawekezaji wa kigeni.
Aidha, imeshauriwa kuzilazimisha kampuni hizo kurejesha nchini asilimia 60 ya
mauzo yake, ili kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni, pamoja na
kuimarisha Shilingi ya Tanzania.
Ushauri huo ulitolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
aliyestaafu, Ludovick Utouh pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Uhamasishaji
wa Uwazi katika mapato ya Madini, Gesi na Mafuta (EITI), Jaji mstaafu Mark
Bomani, wakati wa uzinduzi wa ripoti za kamati za mwaka 2013 na 2014
uliofanyika jana Dar es Salaam.
Akizindua ripoti hizo, Utouh alisema, Tanzania haijafaidika na rasilimali za
madini, jambo lililosababishwa na kujiondoa kufanya biashara, hivyo kuzipa
mwanya kampuni za kigeni kuendesha biashara bila uwazi kuhusu mapato
zinazoyapata kutokana na mauzo ya madini.
“ Serikali iliangalie jambo hili na kulirekebisha, Serikali ya Botswana ina hisa
kwenye migodi hiyo, hivyo wanakuwa na mwakilishi kwenye bodi jambo ambalo
linakuwa rahisi kufuatilia mapato yanayopatikana, lakini sisi hapa tulijiondoa
kwa madai kuwa Serikali haifanyi tena biashara,” alisema Utouh.
Alisema, Serikali ikifanya hivyo itaweza kupata mapato mengi zaidi kuliko ilivyo
sasa, ambapo imejiondoa kabisa katika umiliki wa migodi ilhali rasilimali hizo ni
za Watanzania.
“Wawekezaji wanakuja na fedha na utaalamu, lakini sisi cha kwetu ni rasilimali,
ni lazima tugawane nao na tuwe na mwakilishi kwenye bodi, badala ya kusubiri
mrabaha unaotokana na faida anayopata mwekezaji. Huu utaratibu wa
kuwaachia kila kitu sio mzuri,” alisema Utouh.
Naye Jaji Bomani alisema, Serikali inatakiwa kuzilazimisha kampuni
zinazochimba madini nchini kurejesha asilimia 60 ya mauzo yake ili kuimarisha
akiba ya fedha za kigeni. Alisema, kwa kufanya hivyo, Shilingi ya Tanzania
itaimarika.
Alisema, hatua hiyo ikichukuliwa, sekta ya madini itakuwa imetoa mchango
wake kwa pato la Serikali, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zinazoikabili
sekta hiyo.
Alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni kupanua wigo wa wachimba madini
kama vile wachimbaji wa kati na ambao pato lao linazidi Sh milioni 200, kwa
mwaka ambao, alisema wanastahili kutoa mchango kwa pato la Serikali.
Alisema mpaka sasa ni kampuni kubwa tu zinahusika, lakini akasema umefika
wakati wachimbaji wa kati nao waingizwe kwenye utaratibu huo.
Alipendekeza kuwa umefika wakati sekta ya madini ipanuliwe hadi kwenye
uchimbaji wa makaa kuiwezesha nchi kufaidika zaidi na shughuli za rasilimali
hiyo, ambayo inaweza kuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
EITI ni shirika la kimataifa ambalo liliundwa mwaka 2002 na nchi mbalimbali
zenye sekta ya madini. Linafanya ufuatiliaji juu ya sekta ya madini na gesi na
kuona kama kuna uwazi katika biashara yake.
Tanzania ilijiunga na shirika hilo mwaka 2009. Kazi kubwa ya kamati
iliyoundwa kushughulikia shughuli hizo hapa nchini ilikuwa ni kukusanya taarifa
juu ya malipo ambayo kampuni za madini zilikuwa zinalipa serikali ya Tanzania
na kuzilinganisha na mapato ambayo yalikuwa yamepokelewa serikalini na
kutoa taarifa kila mwaka.

No comments