Wednesday 27April,2016. Ripoti ya CAG Yawaweka Kikaangoni Vigogo wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)

Ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
Profesa Musa Juma Assad imezichanganya Hospitali ya Taifa Muhimbili na
Bohari ya Dawa (MSD), huku Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Ummy Mwalimu akihitaji maelezo ya kina kuhusu mkanganyiko huo.
Ummy ameitaka MSD kuandika maelezo ya kina kwa maandishi, kuhusu vifaa
vya Sh2 bilioni ambavyo viko njiani kwenda Muhimbili kwa miaka minne sasa,
kabla wizara yake haijatoa tamko rasmi.
Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu jana alisema bohari haina mzigo
wowote ulio njiani kuelekea Muhimbili bali imekuwa ikisambaza dawa zake nchi
nzima.
Bwanakunu alisema tatizo lililojitokeza ni mfumo wa kompyuta ambao
unaonyesha mzigo upo njiani, hivyo muamala katika kompyuta unavyoshindwa
kukamilika, mzigo lazima uonekane upo njiani.
“Mwaka 2012 tulibadilisha mfumo wa kompyuta kutoka wa awali mpaka
tunaotumia sasa, hivyo kuna miamala ilihitaji kubadilishwa, mwaka huu
tulifanya zoezi la kukamilisha baadhi na si kwa Muhimbili pekee kwa mfano
kuna mzigo unatoka MSD Ubungo kwenda Muleba ukifika kule mtu anashindwa
kuingiza kwenye mfumo kwamba umepokelewa,” alisema Bwanakunu.
Alifafanua kwamba majibu ya MSD kwa CAG yalieleza kuwa walitengeneza timu
ya uchunguzi na baadhi ya watu walichukuliwa hatua, “nimeshachukua hatua
za haraka baada ya kupata hiyo ripoti, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wale
ambao hawakujaza hiyo miamala tulishawachukulia hatua, hakuna mali
iliyopotea MSD.”
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba kuna ripoti ya Muhimbili ambayo inaonyesha
katika vitabu kwamba kuna mzigo ambao Muhimbili iliununua kutoka MSD,
lakini haujafika, lakini Bwanakunu alipoulizwa alisema hakuna vitabu
vinavyoonyesha kuwa Muhimbili inadai vifaa tiba na dawa MSD.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru
alisema kwa taarifa alizonazo mpaka sasa CAG alifanya ukaguzi katika vitabu
vya MSD na si wao na alipouliza vifaa viko wapi alijibiwa kuwa vinakwenda
MNH.
Alisema kuwa Watanzania wawe na subira na kwamba watapewa majibu kesho
(leo), baada ya Muhimbili kupekua kwa kina vitabu vya mwaka 2012, ili
kujiridhisha iwapo vifaa vilipokelewa au havikuwahi kununuliwa Muhimbili.
“Hiyo ripoti tumeiona leo Jumanne. Hayo mambo yametokea mwaka 2012
huwezi kuwa na jibu la kila kitu, kesho tunataka tukapitie hiyo ripoti kwa
sababu ni ukaguzi wa MSD, tukaangalie vitabu hivyo vifaa vilifika?” Alisema
Museru.
Naye Waziri Ummy Mwalimu alisema katika ripoti hiyo kuna hoja mbili ambazo
ni MSD na TFDA, huku akifafanua kwamba amezungumza na Mkurugenzi wa
MSD lakini hajaridhika na majibu na kumtaka aandike maelezo ya kina.
“Nimetaka maelezo ya maandishi kutoka kwa MSD na TFDA kuhusu ripoti ya
CAG tumekubaliana na Katibu Mkuu walete maandishi ndiyo tutatoa msimamo
rasmi wa wizara, kwa upande wa MSD ndiyo maana tuliweka pembeni wale
wakurugenzi wanne sababu ya changamoto hii ambayo CAG amekutana nayo,”
alisema Ummy.

No comments