Friday, April 29,2016 Spika Apangua tena Kamati za Bunge, Wabunge Wapinga
Spika wa Bunge, Job Ndugai amefanya mabadiliko mengine ya kamati za Bunge
kwa kuwaongeza wabunge wapya na kuwahamisha wengine kwenda kwenye
kamati nyingine, jambo ambalo limepingwa na baadhi ya wabunge wakidai
linapunguza ufanisi.
Juzi, Spika Ndugai (pichani) aliwaongeza wabunge wanne wapya walioapishwa
bungeni Aprili 19, kwenye kamati za Miundombinu; Ardhi, Maliasili na Utalii;
Kilimo, Mifugo na Maji; na Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
Hayo ni mabadiliko ya pili tangu Bunge la 11 lianze rasmi vikao vyake katikati
ya Novemba mwaka jana, ikiwa ni kipindi kifupi cha mabadiliko ikilinganishwa
na Bunge la Tisa na 10.
Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Bunge,
mabadiliko hayo yamefanyika kwa mujibu wa kanuni ya 116 (3) na (5) ya
Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2016, ili kuhakikisha kila mbunge
anakuwa mjumbe wa kamati mojawapo ya Bunge.
“Aidha, mabadiliko haya ni kwa ajili ya kuhakikisha kuwa kadri
itakavyowezekana, Muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge unazingatia aina
za wabunge kwa jinsia, pande za Muungano na Vyama vya Siasa vyenye
uwakilishi bungeni, ujuzi maalumu, idadi ya wajumbe kwa kila kamati na
matakwa ya wabunge wenyewe,” inasema taarifa hiyo.
Baadhi ya wabunge jana walipinga mabadiliko ya mara kwa mara ya wajumbe
wa kamati, wakieleza kuwa hayaleti tija na uamuzi huo haufanywi kwa umakini.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT Wazalendo), alisema mabadiliko
hayo yanaonyesha namna ambavyo Spika Ndugai “anavyokosa umakini katika
uundaji wa kamati hizo”.
“Spika hakuwa makini wakati anaziunda kamati hizo na sina jingine zaidi ya
kusema, maana hilo liko wazi,” alisema Zitto.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema uundaji wa
kamati kila mara, unatokana na kiongozi huyo kutokuwa na umakini na mara
nyingi anafanya kazi kwa shinikizo la vikao vya chama.
Msabaha alisema utaratibu wa kuvunja kamati na kuziunda unatokana na vikao
vya wabunge wa CCM, ambavyo humshauri Spika juu ya nini kifanyike ili
waweze kuubana upinzani, ushauri ambao anadai wakati mwingine unakosa
tija.
Mbunge wa Sengerema William Ngeleja (CCM) alisema mabadiliko
yanayofanywa hayana madhara yoyote, kwa kuwa ni jambo la kawaida kufanya
maboresho na kuwataka wabunge kujifunza kupitia mchezo wa mpira ambao
kila mtu anakuwa na namba yake, lakini uwanjani anacheza namba zote.
“Waangalie mfano wa Profesa Makame Mbarawa ambaye alipewa Wizara ya
Maji, lakini akaondolewa baada ya wiki tatu na kupelekwa kusimamia barabara
ambako ameonyesha uwezo mkubwa, iweje kwa wabunge?” alihoji Ngeleja.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema mabadiliko yanayofanywa
hayawezi kuleta tija katika bunge hilo, kwani watu wanashindwa kujipanga
vyema kwa kuwa hawajui kesho itakuwaje.
Lugola alihoji juu ya mafunzo waliyopata kila kamati, lakini wanabadilishwa bila
utaratibu huku akisema hata kamati ya uongozi inaathirika zaidi, kwani
wanapobadilishwa na kuondolewa wenyeviti lazima kamati ya uongozi ibadilike.
Spika Ndugai hakupatikana jana kueleza kwa kina mabadiliko hayo. Naibu
Spika, Dk Tulia Ackson alisema siyo msemaji na Ndugai na ndiye angepaswa
kuulizwa jambo hilo.
Katika taarifa hiyo ya Bunge, Spika Ndugai aliwataka wajumbe wa kamati sita
ambazo hazina viongozi kuwachagua mapema iwezekanavyo kama kanuni za
Bunge zinavyohitaji.
Kamati hizo ni Hesabu za Serikali (PAC) Mwenyekiti; Kamati ya Nishati na
Madini, (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Ardhi, Maliasili na
Utalii (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Hesabu za Serikali za
Mitaa (Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti); Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya
Umma (Mwenyekiti) na Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Makamu
Mwenyekiti.
No comments