Tuesday, April 26, 2016 Breaking Newa: Rais Magufuli Aivunja Bodi ya TCRA na Kumsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Hiyo Dr Ally Yahaya Simba


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na
kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally Yahaya
Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo
wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza
mapato ya takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu Jijini Dar
es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu
kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya fedha na
Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia mkataba
na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya
simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano lakini mpaka
sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo kinachohusiana na
uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali ambayo imesababisha

serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na
Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais
Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa
Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo
mara moja.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu
Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji
wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya kazi, na nchi
ipate mapato yanayostahili kukusanywa.

“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote
ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yoyote
atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Aprili, 2016

No comments