KILICHOMPONZA BOSS WA TANESCO KUTUMBULIWA NA JPM
HATUA
ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha
mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika
hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla
ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye jana alisali mjini
Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini
Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri
Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Ewura
juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya
Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo
ilisitishwa na Profesa Muhongo. “Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza
hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya
nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu
akae pekee yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka
nyingine,” alisema Rais.
Ateua bosi mpya
Taarifa
iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa
ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua
Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Mwinuka
ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa
jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo
cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
#HabariLeo

No comments