WATU 14 WAFUKIWA NA KIFUSI CHA UDONGO WAKICHIMBA MADINI MKOANI GEITA

WATU kumi na nne akiwemo raia wa China wamefukiwa na udongo usiku wa kuamkia leo majira ya saa saba usiku (7:00) wakiwa wanaendelea na majukumu yao ya uchimbaji madini  kwenye kampuni ya RZ iliyopo kijiji cha Nyarugusu  Mkoa wa Geita.

Inaelezwa kuwa sababu za kuporomoka udongo ni kutokana na mgodi kuchimbwa zamani na Wajerumani hivyo kupelekea baadhi ya maeneo hayo kuwa na nyufa na vyuma kushindwa kushikilia udongo wa juu hali ambayo imepelekea kuzidiwa na hatimaye kuporomoka.

Kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Geita,ikiongozwa na mkuu wa Mkoa huo Meja jenerali mstaafu Ezekiel Kyunga imefika katika Mgodi wa RZ kuangalia na kujionea zoezi la ukoaji .

Kamisha msaidizi wa madini kanda ya ziwa victoria Mhandisi Yahaya Samamba ,ameeleza kuwa jitihada ambazo zimefanyika ni kuwasiliana na migodi iliyopo karibu na eneo hilo na pia wameshaomba msaada kutoka Kahama na kwenye mgodi wa GGM kupatiwa vifaa vya uokoaji ili zoezi hilo liweze kufanikiwa kwa urahisi zaidi.


“Jitihada ambazo tumezifanya hadi sasa tumeomba msaada Kahama na kwenye mgodi wa Geita,kupatiwa vifaa ambavyo vitasaidia kwa wepesi zoezi hili la uokoaji ingawa tumeshapata vifaa vingine kutoka kwenye mgodi wa Busolwa”,alisema Samamba.


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoa wa Geita Elisa Mugisha,amesema eneo la chini ambalo limefukiwa na udongo ndiyo ambalo kwa sasa wanaendelea kulitanua ili sehemu hiyo iwe kubwa watu waweze kupita.

“Eneo lote lile la chini limefukiwa na udongo lakini kule chini kunaonekana kuna sehemu za kwenda pembeni ingawa limefukiwa lakini chini kuna uimara kuna uwezekano kule chini wale watu wapo hai na wamepelekewa mipira ya hewa na kazi inayofanyika ni kutanua eneo ambalo litasaidia kuwatoa watu hao",amesema.


Mwanasheria na msemaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya RZ  Frances Kiganga ameelezea kuwa chanzo kikubwa ni mashimo ya zamani kwani udongo unapotikisika umekuwa ukisababisha baadhi ya nyufa kuendelea kupata shida.


Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo Charles Julius Na Robert Stanley ambao wameeleza kuwa mida ya saa saba usiku duara lilinza kushuka taratibu na baada ya hatari hiyo walipewa taarifa ya watu ambao walikuwa chini kupandisha juu lakini hata hivyo jitihada hizo hazikuzaa matunda.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga amewataka wanaosimamia zoezi la uokoaji kuongeza nguvu ya uokoaji.
Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Elisa Mugisha,akitoa maelezo namna ambavyo wanaendelea na jitihada za kuokoa 
Kamisha msaidizi wa madini kanda ya ziwa victoria Mhandisi Yahaya Samamba ,akifafanua namna ambavyo wameweza kuwasiliana na makampuni mengine ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu waliofukiwa
Moja kati ya wafanyakazi kwenye mgodi huo akielezea hali ilivyotokea na shimo lilivyojifukia
Mkuu wa Mkoa wa Geita Meja Jenerali Mstaafu Ezekiel Kyunga,akiambatana na msemaji wa mgodi huo Frances Kiganga pamoja na kamanda wa zimamoto,Elisha Mugisha wakielekea kwenye eneo ambalo shimo limejifukia. 
Eneo la shimo likiendelea kuchimbwa
Jitihada za uokoaji zikiendelea
Baadhi ya waokoaji 
Shughuli zikiendelea 

Mwanasheria na msemaji wa kampuni ya uchimbaji dhahabu ya RZ Frances Kiganga ,akielezea chanzo cha mgodi huo kujifunika.

No comments