Jaji Mkuu wa Zanzibar Awaapisha Mahakimu na Makadhi Zanzibar.
Na.Khadija Khamis –Maelezo.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman
Makungu amewataka Mahakimu, makadhi na wasuluhishaji wa migogoro ya
kazi kutekeleza majukumnu yao kwa uwadilifu wakizingatia kutoa haki kwa
wanaostahiki kupata haki hizo.
Jaji Makungu
aliyasema hayo katika hafla ya kuwaapisha Makadhi wa Wilaya, Mahakimu wa
Mahakama ya Mwanzo na wasuluhishi na waamuzi wa migogoro ya kazi chini
ya kamisheni ya kazi katika mahakama kuu Vuga.
Aliwaeleza
wasimamizi hao wapya wa sheria kuwa majukumu waliyokabidhiwa na Taifa
sio mepesi na kuwataka kuzingatia maadili ya kazi ili haki na sheria
iweze kuchukua nafasi yake.
Aidha alisema
usuluhishi na utoaji maamuzi panapotokea migogoro katika sehemu za kazi
inasaidia katika kujenga umoja na ushirikiano miongoni mwa
wafanyakazi.
Waliapishwa kuwa
Makadhi wa Mahakama ya Wilaya ni Idi Said Khamis na Sleiman Khamis
Machano, Mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ni Hakimu Amina Mohd Makame na
Hamad Ali Sleiman, wasuluhishaji na waamuzi wa migogoro ya kazi ni
Fatma Abdalla Hamad, Jokha Lali Ramadhani , Juma Ali Makame na Raya
Said Ali .
Akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya sheria duniani ambayo
kilele chake ni tarehe tisa ya kila mwaka, Jaji Mkuu Omar Othman Makungu
alisema shamra shamra za sherehe hiyo zitaanza tarehe nne mwezi ujao
kwa matembezi ya hiari.
Aliongeza kuwa
katika maadhimisho hayo kutakuwa na maonyesho ya sheria, utoaji wa vyeti
kwa mawakili wapya na uzinduzi wa mahakama ya watoto katika kijiji cha
Mahonda Wilaya ya Kaskazi B.
Alifahamisha
kuwa kutakuwa na mikakati ya mipango kazi ambayo itasaidia kufanya kazi
kwa wakati muafaka na kuwepo na utaratibu maalumu wa kuamua kesi ili
kuepuka msongamano wa kesi katika mahakama ili kupunguza malalamiko
kutoka kwa wananchi.
Jaji Mkuu wa Zanzibar alisema kaulimbiu ya siku ya sheria duniani mwaka huu ni kusimamia sheria na maadili katika kutenda haki.
No comments