TAZAMA YATAKIWA KUBANA MATUMIZI ILI KUONGEZA UZALISHAJI
Kampuni ya Kusafirisha Mafuta Ghafi ya TAZAMA imetakiwa kutumia uchumi kushusha gharama za matumizi ili kumudu ushindani wa soko Nchini Zambia.
Wito huo umetolewa hivi karibuni kwa nyakati tofauti na Mawaziri wa Nishati wa Tanzania na Zambia, Profesa Sospeter Muhongo (Tanzania) na Mabumba David (Zambia) walipokuwa wakizungumza na wafanyakazi wa Vituo vya Kusukuma Mafuta (Pumping Stations) vilivyopo Mkoani Mbeya na Iringa wakati wa ziara ya kutembelea vituo hivyo.
Profesa Muhongo alisema dhamira ya Serikali za Tanzania na Zambia ni kuhakikisha Bomba pamoja na Mfumo mzima wa uendeshaji wa kampuni hiyo vinaboreka na kuweza kushusha bei ya mafuta ili kumudu ushindani.
Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) na Waziri wa
Nishati wa Zambia, Mabumba David (nyuma yake) wakikagua Kituo cha
Kusukuma Mafuta Ghafi (Pumping station) cha TAZAMA kilichopo Mkoani
Mbeya.
Alisema
kampuni ya TAZAMA haiwezi kuendelea na utendaji wa kizamani huku
ikitumia gharama kubwa kwenye uendeshaji na hivyo kusababisha kuuza
mafuta yake kwa bei ya juu ikilinganishwa na wauzaji wengine kwenye
soko.
Aliongeza
kwamba zinahitajika jitihada za makusudi kuhakikisha uzalishaji
unaongezeka kwa lengo la kuweza kuingia kwenye ushindani wa soko.
Alisema
teknolojia inayotumiwa na kampuni hiyo kwa ujumla wake imepitwa na
wakati na ili kuongeza uzalishaji ni muhimu kuhakikisha teknolojia hiyo
inaboreshwa sambamba na uboreshwaji wa utendaji wa wafanyakazi wake.
“Hampaswi kuridhika na kiwango mnachosafirisha kwani ni kidogo sana
ikilinganishwa na hapo awali; mkiendelea hivi mnaweza kujikuta
mnasafirisha hata lita laki moja,” alisema.
Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akikagua moja ya
mtambo wa Kusukuma Mafuta Ghafi wa TAZAMA Mkoani Iringa.
Kwa
upande wake Waziri David alisema TAZAMA inapaswa kuelewa dhamira ya
Serikali hizo mbili ili ifanye jitihada ya kufikia malengo hususan
ikizingatiwa kwamba mahitaji ya mafuta nchini Zambia yameongezeka
tofauti na ilivyokuwa hapo awali.
Alisisitiza
kuwa ni lazima kukafanyika mabadiliko ya kiteknolojia na kiutendaji ili
kufikia lengo na alitaja sababu mojawapo inayosababisha mafuta ya
TAZAMA kuuzwa kwa bei ya juu kuliko wengine ni kwamba mafuta
yanayosafirishwa ni machache wakati gharama ya usukumaji wa mafuta hayo
inabaki kuwa kubwa.
“Mkisafirisha
mafuta mengi ni lazima gharama zitapungua na hivyo mtaweza kuuza mafuta
yenu kwa bei ndogo ikilinganishwa na wengine,” alisema.
Waziri wa
Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akizungumza na
wafanyakazi wa Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha TAZAMA kilichopo
Mkoani Iringa. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba
David. Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini,
Profesa Justin Ntalikwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Zambia,
Brigedia Jenerali Emelda Chola.
Aliwaasa
wafanyakazi wa TAZAMA kuwa waelewa na kukubali kubadilika kwa faida yao
binafsi na kwa faida ya nchi za Tanzania na Zambia kwa ujumla.
“Nyie
mtakua sehemu ya mabadiliko na mabadiliko hayo ni kutoka kwenye
Usafirishaji wa Tani 650,000 hadi kufikia Tani milioni 1.1 ambayo ndio
uwezo wa Bomba,” alisema Waziri David.
Alisema kuwa kwa tathmini iliyofanywa ya mahitaji ya mafuta Nchini
Zambia ifikapo Mwaka 2030, itakuwa ni tani milioni 4 na kwa namna
ambavyo kampuni hiyo ilivyo hivi sasa, haitoweza kukidhi soko hilo hivyo
ni vyema ikajipanga kujiboresha.
Mawaziri
hao wapo katika ziara ya kutembelea njia ya Bomba la Mafuta Ghafi la
TAZAMA na Vituo vya Kusukuma Mafuta (Pumping stations) kwenye maeneo
yote linapopita Bomba hilo.
Mfanyakazi
wa TAZAMA katika Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha Iringa, Yerusalem
Anthony akiuliza swali na kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha
kampuni husika mbele ya Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo (wa pili kutoka kulia) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba
David (kulia).
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (wa tatu kutoka kulia
waliosimama) na Waziri wa Nishati wa Zambia, Mabumba David (kushoto
kwake) pamoja na wafanyakazi wa Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi cha
TAZAMA cha Mkoani Iringa.
Moja ya Mtambo (Pampu) wa Kusukuma Mafuta Ghafi wa TAZAMA Mkoani Iringa. Pampu hizo zilifungwa Mwaka 1968
No comments