FOLENI YA WANAUME “WANAOBISHA HODI” DAWATI YAZIDI KUONGEZEKA
| Pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu |
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha
Imebainika kwamba idadi ya wanaume wanaotoa malalamiko yao
dhidi ya wenza wao imeongezeka karibu mara mbili kwa mwaka 2016 ikilinganishwa
na mwaka juzi 2015.
Akitoa taarifa hiyo ofisini kwake Mkuu wa Kitengo cha Dawati
la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu alisema
kwamba idadi hiyo imeongezeka kutoka walalamikaji 34 mwaka 2015 hadi kufikia 63
mwaka 2016 ambapo ni sawa na 48%.
Alisema ongezeko hilo limetokana na kuenea kwa elimu
inayotolewa na askari wa kitengo cha
Dawati kwa watu wa jinsia zote kupitia vyombo vya habari hasa radio
zilizopo jijini hapa. Alisema mbali na radio pia dawati hilo limetoa elimu
kupitia vikao vya wazazi katika shule ya Msingi Osunyai na Shule ya Msingi
Burka zilizopo halmashauri ya jiji la Arusha ambayo imewasaidia wananchi kujua
haki zao na wapi waanzie pindi wanaponyanyaswa ndani ya ndoa zao.
Mkuu huyo wa kitengo cha Dawati la Jinsia na watoto mkoa wa
Arusha alisema wengi wa wanaume hao huwa wanafanyiwa ukatili wa Kisaikolojia
ambapo baadhi ya wenza wao wanaonekana kutowathamini lakini wengine kukataa
kushiriki tendo la ndoa.
“Mbali na Ukatili wa Kisaikolojia pia baadhi yao wanafanyiwa Ukatili
wa kiuchumi ambapo baadhi ya wanawake wenye uwezo kuwazidi waume zao huwa
wakati mwingine wanatoa maamuzi ya kifamilia pengine yakawa na maendeleo lakini
bila kuwashirikisha wenzi wao hali ambayo inawafanya wenzao wabaini kwamba hali
hiyo inatokana na kuzidiwa kipato na hivyo kushindwa kutengua maamuzi au kutoa
ushauri”. Alisema Mkuu huyo wa Dawati.
Mkuu huyo wa Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha alitaja
wilaya inayoongoza kwa idadi ya wanaume kuripoti malalamiko yao katika ofisi
yake ni Arusha ambayo ilikuwa na jumla ya walalamikaji 48, Arumeru 8, huku Ngorongoro
ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na walalamikaji watatu. Wilaya ya Longido ni
ya nne ambayo ilikuwa na walalamikaji wawili huku Karatu na Monduli zilikuwa
zina mlalamikaji mmoja kila wilaya.
Mkuu huyo wa Dawati alitoa wito kwa viongozi wa kata, mitaa,
vijiji na hata vitongoji kuiarifu ofisi yake pindi wanapokuwa na vikao katika
maeneo yao ili waweze kuzidi kusambaza elimu ya ukatili wa kijinsia kwa
wanandoa kupitia vikao hivyo kwani wanaume wengi awali walikuwa hawana ufahamu
kama wao pia wanaweza kutoa malalamiko yao kupitia dawati hilo.
Ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha mwishoni
mwa mwaka jana imekuwa ikitoa elimu ya ukatili wa jinsia kwa wanafunzi wa shule
mbalimbali za msingi zilizopo katika halmashauri ya jiji la Arusha ambazo ni
Sombetini, Osunyai,Ngarenaro, Kaloleni, Burka na Elerai hali ambayo imewasaidia
wanafunzi hao kupata uelewa mkubwa juu ya ukatili.
No comments