Watu wawili watiwa mbaroni kwa kusababisha kifo mjamzito

Watu  wawili wakazi wa kijiji cha Itagata tarafa ya Itigi wilayani Manyoni mkoani Singida, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kufanya uzembe wa kumchelewesha Heleni Maduhu (29), kitendo kilichosababisha afie  kwenye duka la madawa muhimu.

Watuhumiwa hao ni mume wa Heleni, Bahame Kamuda (32) na mmiliki wa duka la dawa muhimu, Joseph Hengwe.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Debora Magiligimba, alisema tukio hilo limetokea Januari, 25 mwaka huu saa 9:30 alasiri  huko katika kijiji cha Itagata wilaya ya Manyoni.

Alisema Januari, 24 mwaka huu saa nne asubuhi Heleni alipelekwa na mume wake Bahame  kwa usafiri wa pikipiki katika zahanati ya kijiji cha Itagata kufanyiwa uchunguzi wa ujauzito wake.

“Muuguzi Grace Simon baada ya kumfanyia uchunguzi,ilibainika njia ya uzazi bado haijafunguka na hivyo kuwashauri warudi nyumbani.Lakini ilipofikja saa 4.00 asubuhi hali yake iliendelea kuwa mbaya na ndipo mume alipoamua kumpeleka katika zahanati ya misheni kijiji cha Mitundu, kwa matibabu zaidi,” alisema.

Debora alisema lakini wakiwa njiani, aligundua hali ya mke wake kuwa mbaya zaidi na kuamua kumpeleka kwenye duka la dawa muhimu lililopo katika kitongoji cha Kululumo.

“Heleni wakati akienaendelea kupatiwa matibabu katika duka hilo,hali yake iliendelea kuwa mbaya zaidi, lakini aliweza kujifungua mtoto wa kiume salama kwa njia ya kawaida. Baada ya kujifungua damu nyingi zilianza kumtoka,” alisema.

Kamanda huyo alisema Bahame baada ya kuona mke wake akitoka damu nyingi, aliamua tena amkimbize  kutibiwa katika hospitali ya misheni ya Itigi kwa pikipiki, lakini mwanamke huyo alifia njiani.

Alisema kwa sasa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na ofisi ya mganga mkuu wa mkoa wa Singida, kufanya uchunguzi ikiwemo kubaini uhalali wa mmiliki wa duka hilo kutoa huduma kwa mgonjwa

No comments