HOSPITALI ZOTE ZA MIKOA KUWA NA WATAALAM WA MIFUPA
Na: Frank shija -
MAELEZO
WATAALAM wa mifupa
wamepelekwa katika Hospitali zote za Kanda na mataraji ya baadaye ni kuwapeleka
katika Hospitali za Mikoa ikiwa ni kusogeza huduma za tiba ya mifupa karibu
zaidi na wananchi.
Hayo yamebainishwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Mpoki Ulisubisya katika kipindi cha TUNATEKELEZA kinachorushwa na kituo cha
luninga cha TBC1 kwa kushirikiana na Idara ya Habari MAELEZO jana jijini Dar es
Salaam.
Dkt. Ulisubisya amesema
kuwa wataalamu hao wamepelekwa katika Hospitali hizo ili kutatua changamoto ya
matibabu ya magonjwa ya mifupo yaliyoongezeka kwa wingi kutokana na ajali hasa
zitokanazo na Bodaboda.
“Serikali imepeleka
Wataalamu wa mifupa katika Hospitali za Kanda ikiwa ni njia ya kusogeza huduma
za matibabu ya mifupa karibuzaidi na wananchi kwani kumekuwa naongezeko la
wagonjwa kutokana na ajali hasa za Bodaboda” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha Katibu Mkuu huyo
amesema kuwa pamoja na kupeleka wataalamu wa mifupa katika Hospitali za Kanda
na mikoa, mikakati ya Serikali ni kuhakikisha huduma za Afya zinakuwa bora na
zinawafikia wananchi kwa urahisi ndiyo maana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imekuja na dhana ya kuwa na Zahanati kila
Kijiji ambazo zitapatia dawa na vifaa tiba muhimu.
Aliongeza kuwa katika
kuhakikisha dhana hiyo inatekelezeka Wizara ya Afya imekuwa ikishirikiana na
TAMISEMI ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia huduma, kuhakikisha huduma za
msingi zinapatikana ikiwemo miundombinu ya Zahanati, Vituo vya Afya na
Hospitali pamoja na Dawa na Vifaa Tiba.
“Pamoja na kuwa mambo
mengine yanasimamiwa na TAMISEMI lakini ninapokuwa katika ziara nikikutana na
changamoto zinazowahusu nashughulikia kisha nawapa taarifa ili wachukue hatua
stahiki, hivyo ndivyo tunavyoshirikiana katika kuhakikisha wananchi wanapata
huduma bora za Afya.”Alifafanua
Kuhusu upatikanaji wa
dawa Dkt. Ulisubisya
amesema kuwa hadi kufikia mwezi wa tano upatikanaji wa dawa utakuwa umefikia
asilimia 90% kutoka 70% za sasa na kuongeza kuwa suala la dawa limepewa
kipaumbele katika bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/2017 ambapo takribani
shilingi 251 bilioni zimetengwa kwa ajili ya dawa na vifaa tiba.

No comments