Waziri Ummy Mwalimu Azindua Huduma Mpya ya Kupandikiza Vifaa vya Usikivu Muhimbili, apiga Marufuku Wagonjwa Kutibiwa Nje ya Nchi
Serikali
imesema kwamba kuanzia sasa haitapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili
ya kupandikiza vifaa vya usikivu kwa kuwa huduma hiyo imeanza kutolewa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kauli
hiyo imetolewa Leo na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Mheshimiwa Ummy Mwalimu katika hospitali hiyo wakati
akizindua huduma ya upasuaji wa kupandikiza vivaa vya usikivu (Cochlea
Implant).
Ummy
alisema kuwa huduma hizo zitakuwa zikitolewa Muhimbili kwa sababu ina
madaktari bingwa wenye uwezo wa kufanya upasuaji huo na vifaa vya kisasa
na kuokoa gharama kubwa ambazo zilikuwa zikitumika awali kupeleka
wagonjwa nje ya nchi.
Waziri
huyo amesema katika hospitali za umma, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza
kutoa huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu na ya pili kutoa
huduma hiyo katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki ikitanguliwa na
Kenya.
“Nafarijika
Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutoa huduma hii kupitia hospitali ya umma
ambayo ni Muhimbili yenye hadhi ya ubingwa wa hali ya juu.
Wenzetu
Kenya huduma hii inatolewa kwenye hospitali binafsi na inakadiriwa
kugharimu dola 31,000 za Marekani ambazi ni sawa na Sh69 milioni za
Kitanzania. Hivyo basi tuna kila sababu ya kujipongeza kwa hatua
tuliyofikia,”
Akizungumzia
gharama, Waziri amesema kuwa mgonjwa mmoja itamgharimu Sh36.9 milioni
kwa ajili ya upandikizaji wa kifaa cha usikivu na kwamba kutolewa kwa
huduma hiyo katika Hospitali ya Muhimbili itasaidia kupunguza gharama za
matibabu kwa zaidi ya asilimia 60.
Amesema
fedha za matibabu zitakazokuwa zikilipwa Muhimbili zitakuwa zikitumika
kulipia matibabu kwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo.
“Ikumbukwe kwamba
serikali ilikuwa ikigharamia Sh80 milioni hadi 100 kwa ajili kupandikiza
kifaa cha usikivu kwa mtoto mmoja aliyekuwa akipelekwa kutibiwa nje ya
nchi,”amesema.
Ummy
amesema kuwapo kwa huduma hizo nchini kutawawezesha Watanzania wengi
kutibiwa na kuipunguzia serikali gharama ya kupeleka wagonjwa nje
kutibiwa na kwamba gharama zitapungua kwa zaidi ya asilimia 60.
Waziri
huyo amesema kuwa wagonjwa wasiokuwa na uwezo wa kifedha watapatiwa
huduma hiyo kupitia sera ya msamaha kwa watu wasiokuwa na uwezo.
“Hospitali ya Muhimbili ina utaratibu mzuri wa kutoa huduma kwa wagonjwa
wote wasiokuwa na uwezowa kulipia. Ni vyema wananchi wakatumia
utaratibu huo badala ya kukimbilia kwenye vyombo vya habari
kulalamika,” amesema waziri huyo.
Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili kwa siku mbili mfulilizo kuanzia tarehe 5 hadi 6
Juni, 2017 kwa kushirikiana na wataalamu kutoka India na Misri
wamefanikiwa kufanya upasuaji kwa watoto watano ambao walizaliwa wakiwa
na matatizo ya kutosikia.
Katika
hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence
Museru amesema kuwa tatizo la usikivu limekuwa likiongezeka katika jamii
na kwamba endapo watoto watabainika kuwa na tatizo hilo mapema na
kuwekewa vifaa vya usikivu (Cochlear Implant) wataishi kama watu
wengine ambao hawana matatizo na kwamba wasipowekewa vifaa hivyo
watakuwa viziwi.
"Ufafiti wa Hospitali ya Muhimbili unaonyesha kuwa kwa
mwaka karibu watoto 300 hadi 400 wanahitaji huduma hii hapa nchini.
Tunaamini kuwa kuanzishwa kwa huduma hii nchini itawanufaisha wengi,”
amesema Profesa Museru.
Profesa
Museru ameomba Muhimbili iungwe mkono katika juhudi zake za kuboresha
huduma na kwamba iwapo mpango wa kupata madaktari na wauguzi kutoka Cuba
utakapokamilika utasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje.
“Tunaomba
Serikali itufikirie sisi Muhimbili katika kuwezesha huduma hizi kuwa
endelevu kwa kutenga kiasi cha fedha za kutosha ili kuwalipia Watanzania
ambao wanahitaji huduma ya upandikizaji wa vifaa vya usikivu,” amesema
Profesa Museru Leo.
Pia,
Profesa Museru amefafanua kuwa gharama zilizotumika kwa ajili ya
kukarabati, ununuzi wa vifaa tiba, kusomesha wataalamu nje ya nchi,
kupanua miundombinu ya utoaji huduma zimegharimu jumla ya Sh13.664
bilioni na kwamba Sh8.855 bilioni zilitumika kununua vifaa vya tiba, Sh
3.858 kwa ajili ya ukarabati na Sh850 milioni kwa ajili ya kusomesha
wataalamu.

No comments