Rais Magufuli Atuma Salam Za Rambirambi Kwa Klab Ya Yanga Na CCM Kwa Kifo Cha Ally Yang



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), uongozi wa Klabu ya Yanga na wanamichezo wote kwa ujumla kufuatia kifo cha shabiki mkubwa wa timu ya Yanga Bw. Ali Mohamed maarufu kwa jina la Ali Yanga.

Ali Yanga amefariki dunia jana tarehe 20 Juni, 2017 kwa ajali ya gari iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo kilichopo katika Wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma.

Mhe. Rais Magufuli atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo wake na mchango wake wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa michezo, ikiwemo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya Taifa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa Uhuru na ziara za viongozi.

“Nimeguswa sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa nae wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo alitoa mchango mkubwa katika uhamasishaji wa wananchi kukipigia kura chama changu cha CCM, na pia amekuwa akiongoza mashabiki wenzake kuishabikia timu ya Yanga na timu ya Taifa bila kuchoka. Kwa kweli alikuwa hodari sana katika ushabiki wake.

“Natoa pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa timu ya Yanga, wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha Ali Yanga na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kibaha, Pwani.
21 Juni, 2017

Shabiki wa Yanga maarufu kwa jina la Ally Yanga amefariki dunia jana  katika ajali ya gari. Ally Yanga alijizolea umaarufu mkubwa katika tasnia ya soka kotokana na jinsi alivyokuwa akivaa na kujichora pamoja na namna yake ya ushangiliaji anapokuwa uwanjani.

Ajali hiyo iliyohusika katika kifo cha Ally Yanga iiltokea jana  mkoani Dodoma

Klabu ya Yanga kupitia Idara ya Habari na mawasiliano wametuma salamu za rambirambi kwa ndugu na jamaa wa Ally Yanga kufuatia kifo cha mpendwa wao ambapo wamesema kuwa faraja ya Mungu ikawe na familia hiyo katika kipindi hiki kigumu.

“Uongozi wa Yanga SC umepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Ally Yanga, hakika Mungu ni mwema, faraja ya Mungu wetu ikawe kwa familia katika kipindi chote cha majonzi kwa kuondokewa na mpendwa wao.”

Aidha, kwa upande wao, Yanga wamesema kuwa wameachwa na pengo kubwa kutokana kutokana na kupoteza shabiki na mwanachama huyo maarufu.

“Pia nasi Yanga kifo chake kina acha pengo kubwa kwa nafasi yake ambayo ilipelekea kujipatia umaarufu mkubwa na alikuwa balozi mzuri kama mwanachama na shabiki mkubwa wa timu yetu, Bwana alitoa, Bwana ametwaa.”

No comments