Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka wazidi kushika kasi jijini Dar es salaam
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald
Rwakatare akiwasili katika Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka cha
Kimara Mwisho. Mhandisi Rwakatare alipokewa na Kaimu Meneja Usafirishaji
wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dkt Philemon Mzee (kushoto).
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald
Rwakatare akipita sehemu ya ukaguzi wa tiketi na kadi zitumiwazo na
Mabasi Yaendayo Haraka. Mhandisi Rwakatare alipata fursa ya kutembelea
vitengo mbalimbali vya Kituo Kikuu cha Kimara mwisho na kujionea huduma
za usafiri zinavyofanyika katika kituo hicho.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald
Rwakatare akizungumza na mmoja wa abiria wa Mabasi yaendayo haraka
katika Kituo Kikuu cha Mabasi hayo katika eneo la Kimara Mwisho.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald
Rwakatare (kulia) akitembelea vitengo mbalimbali vya kutoa huduma katika
Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo haraka kilichopo Kimara mwisho.
Mhandisi Rwakatare aliambatana na Kaimu Meneja Usafirishaji wa DART Dkt
Philemon Mzee, na Kushoto ni Afisa Habari Mkuu wa DART bwana Mathew
Kwembe.
Sehemu
ya daraja linalotumiwa na wananchi pindi wanapoingia na kutoka katika
Kituo Kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka kilichopo Kimara Mwisho. Daraja
hili ni miongoni mwa miundombinu iliyojengwa na Serikali kwa ushirikiano
na Benki ya Dunia.
Na Mathew Kwembe
Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) Mhandisi Ronald
Rwakatare ameeleza kuwa mradi huo umepata mafanikio makubwa katika
kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es salaam hususani katika
barabara ya Morogoro.
Akizungumza
na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea kituo kikuu cha Kimara
mwisho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma,
Mhandisi Rwakatare alisema kuwa katika kipindi hicho cha mpito, Mabasi
yaendayo haraka yameweza kusafirisha watu 200,000 kila siku kutoka watu
50,000 iliyokuwa ikisafirisha mwaka jana, wakati mradi unaanza.
Mhandisi
Rwakatare alieleza kuwa Mradi huo umeweza kuokoa muda wa wananchi ambao
kabla ya mradi kuanza walikuwa wakitumia usafiri mwingine uliokuwa
ukichukua kutoka masaa mawili, wakati sasa wanatumia dakika 45 tu kwa
safari ya kutoka Kimara hadi Posta kwa kutumia mabasi yaendayo haraka.
Alifafanua
kuwa huduma hiyo mbali na kuwapunguzia mzigo wa nauli watumiaji wa
kawaida wa mabasi ya daladala, mradi wa mabasi yaendayo haraka imeokoa
gharama ya usafiri kwa wenye magari binafsi ambapo wengi wao wamekuwa
wakiutumia zaidi usafiri huo.
Akizungumzia
kuhusu maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma Mhandisi Rwakatare
alisema kwa wakala umeona ni vyema kutumia maadhimisho hayo kusikiliza
kero na maoni ya wananchi hasa watumiaji wa huduma hiyo ili kuona namna
nzuri ya kuiboresha.
“Watumishi
wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka wamekuwepo katika vituo vya
Gerezani na Kimara mwisho kwa siku hizi mbili ili kusikiliza kero na
maoni kutoka kwa wananchi wetu, na tunafurahi kuona huduma hii ikizidi
kushika kasi, hasa kwa kuzingatia kuwa tupo katika kipindi cha mpito,”
alisema.
Hata
hivyo alisema kuwa maoni na ushauri walioupata kutoka kwa wananchi
wataufanyia kazi na kurekebisha kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika
kipindi cha mpito ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa bora zaidi.
Aisema
kuwa Wakala upo mbioni kumpata mtoa huduma ya ukusanyaji mapato ambapo
ndiye atakuwa na jukumu la kushughulikia suala la kadi ili kuondokana na
changamoto mbalimbali za usafiri zinazowakabili watumiaji wa mabasi
hayo.
“Natambua
kuwa kadi zimeisha na wakala unalishughulikia jambo hili na
tutahakikisha kuwa tunaongeza kadi, nawasihi wananchi watambue kuwa tupo
katika kipindi cha mpito, mapungufu mengi yaliyojitokeza
tutayarekebisha,” alisema.
Mhandisi
Rwakatare alibainisha kuwa suala la kadi limechukua muda mrefu kwa vile
mchakato wake unahusisha mfumo wa kibenki na hivyo kuwataka wananchi wa
jiji la Dar es salaam kuwa na uvumilivu katika kipindi hiki cha mpito
kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza hususani suala la kadi
ambapo aliahidi kulitafutia ufumbuzi suala hilo mapema iwezekanavyo.
Mhandisi
Rwakatare alisema kuwa Mradi huo unatekelezwa kwa ubia baina ya
Serikali na Kampuni binafsi ya UDART ambayo ndiyo iliyopewa jukumu la
kutoa huduma ya usafiri wa mabasi yaendayo haraka katika kipindi hiki
cha mpito
Alisema
Serikali kwa upande wake imeshirikiana na Benki ya Dunia kujenga
miundombinu mbalimbali inayotumiwa na mabasi hayo ambapo katika awamu ya
kwanza ujenzi wake umehusisha barabara zenye jumla ya kilometa 20.9
ambazo ni Kimara – Kivukoni, Magomeni – Morocco na Faya – Karikaoo.
Pia
alisema kuwa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka upo mbioni kumpata mtoa
huduma kamili baada ya kipindi cha mwaka mmoja cha mpito. Alisema kuwa
Wakala unatarajia kuongeza mabasi mengine 165 kwa ajili ya kutoa huduma
zaidi za usafiri katika jiji la Dar es salaam.
Alisema kuwa wakala unatarajia kuongeza njia za mrisho katika maeneo ya Mwenge, Kawe na Mabibo.
Mradi
wa Mabasi Yaendayo Haraka ulianza rasmi tarehe 16 Mei, 2016, ambapo
umekwishatimiza mwaka mmoja katika kipindi cha mpito tangu kuanza
kutolewa kwa huduma hiyo ambapo zimepangwa awamu sita za ujenzi wa
miundombinu ya mradi huo katika maeneo mengine ya jiji la Dar es salaam
huku awamu ya kwanza imekwishakamilika.
No comments