Maadhimisho Siku ya Mtoto wa Afrika: Viongozi wa Dini Wakemea Ukatili
Viongozi wa Dini wamekemea vitendo vya ukatili kwa
watoto na kwani vimekemewa hata katika vitabu vya dini, huku wakimtaka
kila mmoja kumlinda mtoto pamoja na kueneza elimu ya malezi. Viongozi
hao walioshiriki katika mkutano wa vyombo vya habari ulioandaliwa na
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kutoka Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa
pamoja waliungana na TAMWA kukemea vitendo vya kikatili wanaofanyiwa
watoto, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika.
Akizungumza Mwakilishi kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA), Sheikh Shomari Mchongoma alisema jamii kwa pamoja inapaswa
kuungana na kukemea vitendo vya kikatili kwani ni kinyume cha imani
zetu. Alisema jambo pekee ambalo linaweza kufanikisha mapambano hayo ni
jamii kumrudia mwenyezi Mungu na kukemea vitendo viovu anavyochukizwa
navyo.
“…Wakati umefika tuangalie ni namna gani kumkomboa mtoto wetu kwenye
wimbi la mateso ya kikatili ambayo wamekuwa wakitendewa baadhi ya watoto
wetu. Mtoto anaweza kuwa salama endapo tutaungana na kukemea vitendo
hivyo bila kujali tofauti zetu,” alisema Sheikh Mchongoma.
Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Bw. Lucas Singili alisema mtoto anaitaji malezi ya pamoja kwa
ushirikiano ikiwa ni kuwaweka karibu ili waweze kukua katika malezi
mema. Watoto hawapaswi kutengwa wala kufanyiwa vitendo vya kikatili
zaidi ya kuwapa msaada kutoka kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla ili
waweze kuwa raia wema wenye maadili katika taifa la baadaye.
Aidha aliongeza kuwa mtoto hapaswi kuchokozwa kwa nmna yoyote kama
wanavyofanyiwa ukatili na mambo yasio mema na baadhi ya watu.Alisema
hata vitabu vya dini vimekemea aina yoyote ya uchokozi dhidi ya watoto,
hivyo kuiomba jamii kushirikiana katika kutoa elimu ya malezi mema kwa
watoto waje kuwa raia wema na bora baadaye. “…Mtoto achokozwi,
usimchokoze mtoto hata maandiko ya dini yanasema hivyo…,” alisisitiza
Bw. Singili wa CCT.
Naye Mtaalamu wa Saikolojia ya Jamii, John Ambrose akizungumza na
wanahabari katika mkutano huo, alisema yapo madhara makubwa yanayomtokea
mtoto endapo akipitia katika vitendwa vya unyanyasaji. Alisema mtoto
anapokumbana na vitendo vya unyanyasaji anapoteza matumaini kwa jamii,
anapoteza imani, anajenga hofu na thamani yake inashuka hivyo kuishi
katika maisha mabaya zaidi.
Alieleza kuwa, mtoto anayefanyiwa vitendo vya kikatili asipo
badilishwa huenda akawa mkatili zaidi hapo baadaye jambo ambalo tunaweza
kujikuta tunaandaa taifa hatari, hivyo kumtaka kila mmoja katika nafasi
yake kukemea vitendo vya kikatili dhidi yao ili kumlinda mtoto.
No comments