Watanzania washauriwa kuchangamkia fursa ya kwenda kuhiji Israel
Mkurugenzi
Mtendaji Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bibi Devota Mdachi, amesema
jijini jana kuwa wadau wa utalii wa Israel wangependa kuona Watanzania
wanatembelea Israel.
Bibi
Mdachi akiongozana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii
Dkt. Aloyce Nzuki ambaye alikuwa kiongozi wa msafara, walitembelea
Israel kwa siku tatu, walikutana na na wadau wa sekta ya utalii na
kuwaeleza vivutio vilivyopo nchini.
“Tumetembelea
maeneo mengi ya kiroho ikiwemo miji ya Nazareth na Jerusalem, wenyeji
wetu wamenipa ujumbe kuwa wanahitaji Watanzania waende wakahiji katika
maeneo hayo kwa bei nafuu inayokadiriwa kuwa kati ya Dola za Kimarekani
1700 na 1800.
“Fursa
hii ni nzuri tafadhali tusiiache kwa sababu mbali ya hija lakini kuna
mambo mengi mengine.
Watakaokwenda watakutana na raia wa mataifa
mengine watawauliza kuhusiana na Tanzania, maana yake mtageuka mabalozi
wetu na kuvutia watalii wengi zaidi,” alisema Bibi. Mdachi.
Alibainisha
kuwa kiasi hicho cha Dola 1700 au 1800 kinahusisha nauli ya kwenda na
kurudi, malazi pamoja na ziara ya maeneo matakatifu ndani ya miji
husika.
“Kampuni
ya Another World imeahidi ifikapo Agosti mwaka huu wataleta watalii
kutoka Israel watakaotembelea maeneo ya Hifadhi ya Katavi, Mahale,
Ngorongoro na Zanzibar.
Mmiliki wa kampuni ya Another World, Bw Shlomo Carmel ameahidi kuleta watalii zaidi ya 2000 kati ya Agosti na Disemba mwaka huu.
Vilevile
kuna wawekezaji katika sekta ya hoteli za viwango vya kimataifa
wameahidi kuja kuwekeza nchini, kifupi imekuwa ni ziara yenye tija kwetu
sote,” alibainisha Bibi. Mdachi.
Balozi
wa Tanzania nchini humo Balozi Job Massima, amesema mbali ya ugeni
wake katika nchi ya Israel amebaini kuna kuna fursa nyingi za kiutali
zinazoweza kunufaisha pande zote.
“Huu
ni mkusanyiko wangu wa kwanza hapa nchini tangu niwasilishe hati zangu
za ubalozi, lakini nimeona namna Waisrael wanavyoipenda Tanzania, nami
nimeona namna vivutio vilivyopo hapa vinavyofaa kwa Watanzania kuja
kutalii.
“Tunasema
hii ni nchi takatifu, waumini wa dini zote duniani wanaguswa na namna
moja au nyingine kuja kuitembelea.
Hivyo nitatumia nafasi yangu ya
ubalozi kuwa kiunganishi kwa Tanzania na Israel kwenye sekta hii muhimu
ya utalii,” amesema Bw. Massima.
Utalii
ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya mapato nchini, ambapo mwaka jana
sekta ya utalii iliingiza kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 2 ikiwa
ni sawa na Sh Trilioni 4, mwaka 2015 iliingiza Dola bilioni 1.9.
Kiwango
hicho cha mapato kiliifanya sekta ya utalii kuchangia asilimia 17.5 ya
pato la taifa katika bajeti ya mwaka 2016/17 pamoja na kuingiza asilimia
25 ya fedha za kigeni.
No comments