JINSI WABUNGE WA UPINZANI WALIVYOSUSA KIKAO CHA BUNGE DODOMA
Mbunge wa Kibamba, John Mnyika ametolewa nje ya Bunge leo Ijumaa kwa agizo la Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Licha ya adhabu hiyo, amemzuia kutohudhuria vikao vya Bunge kwa siku saba kuanzia leo.
Mnyika ametolewa baada ya mmoja wa wabunge kusema 'Mnyika mwizi'
akimhusisha na wizi wa madini, hoja inayochangiwa na wengi kwenye
mjadala wa Wizara ya Nishati na Madini unaoendelea.
Kutokana na hali hiyo Mnyika alimtaka Spika kuchukua hatua kwa mbunge
aliyesema kuwa yeye ni mwizi lakini Spika akasema hajui hilo na
haijaingia kwenye hansadi. Hata hivyo Mnyika alisisitiza kuwa mambo
hayaweze kwenda hivyo.
Baada ya majibizano kati yake na Spika, Spika akaamuru walinzi wamtoe
Mnyika nje ya Bunge na asihudhurie vikao saba vinavyofuata.
Mnyika alikuwa akitoa maelezo baada ya Mbunge wa Mtera, Livingston
Lusinde kusema upinzani wa Tanzania ni wa ajabu kwani unatetea wezi wa
madini.
Baada ya hatua hiyo, wabunge wa upinzani waliamua kutoka nje kupinga mnyika kutolewa nje.
Wakiwa nje ya ukumbi wa bunge, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya
alizungumza na waandishi wa habari na kusema hawakubaliani hatua
iliyochukuliwa na spika dhidi ya mwenzao kwani kuna mbunge wa CCM
alisema wabunge wengine hawana akili lakini hakuchukuliwa hatua yoyote.
“Nadhani hata nyinyi mmeona mbunge aliyekuwa anachangia anasema kuwa
wabunge wengine wapimwe akili, inawezekana hawana akili anaachwa kwa
sababu tu ni mbunge wa Chama Cha Mapinduzi.”
Aidha, Bulaya alisema kazi ya upinzani ni kuikosoa serikali pale mambo
yanapokuwa hayaendi sawa ni si kupongeza kila kitu. Alifafanua zaidi
kuwa hawawezi kuwa wanaisifia tu serikali, bali watafanya hivyo pale
panapopasa kama kwenye wizara ya ardhi ambapo walimpongeza waziri kwa
kazi kubwa anayofanya.
“Msimamo wetu kama Kambi ya Upinzani tumeamua kutoka kwa sababu hatuwezi
kujadili mambo ya msingi kwa kufanyiwa mambo haya, sisi kazi yetu ni
kuishauri serikali lakini hatuwezi kuishauri serikali vile wanavyotaka
wao.
Kwenye Wizara ya Ardhi mbona wabunge wa upinzani walisimama na
wakapongeza na Wizara ya Ardhi ilipita bila shida yoyote kwa pande zote
mbili, sasa kwanini wao wanataka kupongezwa tu? Kazi yetu ni kuona pale
ambapo mambo hayaendi sawa kwa mujibu wa sheria tunasema na hili liwe
wazi watu waliokuwa wakipigia kelele mikataba mibovu ni upinzani
bungeni” alisisitiza Ester Bulaya.
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Maadili itamjadili Mbunge Esther Bulaya kwa kosa la kushawishi wenzake kutoka nje.
No comments