Rais Magufuli apokea taarifa ya Ujenzi wa Bomba la mafuta kutoka Uganda hadi bandari ya Tanga.
Makamu wa Rais wa Kampuni ya Total Afrika Mashariki Bw. Javiero Rielo
amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka
Hoima nchini Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania yanaendelea vizuri
na kwamba kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa
mafanikio.
Bw. Javiero Rielo amesema hayo jana tarehe 24 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es
Salaam alipokutana na Rais Magufuli kwa lengo la kumpa taarifa juu ya
maendeleo ya maandalizi ya kuanza kwa ujenzi wa bomba la mafuta.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 1,410 ambalo
litasafirisha mafuta ghafi kutoka ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya
Tanga nchini Tanzania na unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja 1,500
na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000.
Gharama za mradi wa ujenzi wa bomba hilo zinatarajiwa kuwa takribani Dola
za Kimarekani Bilioni 4 na Kampuni ya Total inasema fedha hizo zipo tayari.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amesema anaamini
kuwa mradi huo utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania, Uganda,
Kampuni ya Total na nchi jirani.
Amebainisha kuwa pamoja na kwamba Tanzania ipo katika mazingira mazuri ya
kutekeleza mradi huo, Serikali yake itatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha
mradi huo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea hati za utambulisho kutoka kwa
mabalozi watatu wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini.
Mabalozi waliowasilisha hati zao ni Mhe. Ian Myles – Balozi wa Canada hapa
nchini, Mhe. Prasittiporn Wetprasit – Balozi wa Thailand hapa nchini mwenye
makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya na Mhe. Harald Gunther – Balozi wa
Austria hapa nchini mwenye makazi yake Mjini Nairobi nchini Kenya.
Pamoja na kuwasilisha hati zao za utambulisho Mabalozi hao wameelezea
kufurahishwa na mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi zao na
Tanzania na wameahidi kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Tanzania ili
wananchi wa pande zote wanufaike na matokeo ya ushirikiano huo hususani
katika uwekezaji na biashara.
Kwa upande wake Rais Magufuli amewahakikishia Mabalozi hao kuwa Serikali
yake itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hizo na
ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishawishi zaidi nchi zao na wawekezaji
katika nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa viwanda, uongezaji
thamani ya madini, kuendeleza kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji,
uzalishaji wa nishati na biashara mbalimbali.
Pia Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi wa Thailand na Austria kuanzisha
ofisi za Ubalozi hapa nchini ili kurahisisha na kuharakisha shughuli za kibalozi.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
24 Agosti, 2016
No comments