Paul Makonda aitwa Tume ya Haki za Binadamu Kujieleza.....Ni kwa kauli yake aliyotoa Agosti 25 Akiwataka Polisi Wawapige Watu Wakiwakuta Msituni


Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa na
matamshi ya Mhe. Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
yanayokiuka misingi ya utawala bora aliyoyatoa tarehe 25 Agosti, 2016 wakati
wa kuaga miili ya askari Polisi watatu waliouawa Mbande, Mkoani Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Bahame Tom Nyanduga, leo (Agosti
26, 2016) Mhe. Makonda ametumiwa barua ya wito inayomtaka afike makao
makuu ya Tume mtaa wa Luthuli, tarehe 30 Agosti, 2016 ili kujadili kile Tume
ilichokiona kuwa ni kejeli kwa Tume pamoja na jumuiya yote ya watetezi wa
haki za binadamu.
Aidha, Tume imeona kuwa maagizo aliyoyatoa Mkuu huyo wa Mkoa kwa Jeshi
la Polisi hayana msingi wa kisheria na hayako ndani ya mamlaka ya Mkuu wa
Mkoa.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia Kifungu cha 27(1) na (2) (a) vya
Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sura Na. 391 ya Sheria
za Tanzania 2002, THBUB ina mamlaka ya kuchunguza mwenendo wa mtu au
taasisi yoyote kuhusiana na utendaji wa kazi zake zinapokiuka mipaka ya
madaraka yake, ili kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji huo.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Agosti 26, 2016






No comments