Uchaguzi Kenya 2017: Matokeo ya urais yaendelea kutangazwa
Kura zinaendelea kuhesabiwa na matokeo kutangazwa baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Jumanne.
Kura ambazo zilikuwa zimeharibika kufikia wakati huo ni 149, 634.
Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo.
Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.
Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa.
Wengi wanahofia uwezekano wa kutokea tena kwa ghasia za baada ya uchaguzi sawa na ilivyotokewa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Watu zaidi ya 1,100 walifariki na wengine 600,000 kuachwa bila makao.
Ili kushinda, mgombea urais anahitajika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa, na angalau asilimia 25 katika kaunti 24 kati ya kaunti 47 nchini humo.
Iwapo hakuna mgombea atakayetimiza hilo, basi uchaguzi wa marudio utafanyika katika kipindi cha siku 30.
Kujitokeza mapema
Wapiga kura walianza kujitokeza alfajiri na mapema kupiga kura.Foleni ndefu zilishuhudiwa katika vituo vingi, na kwingine visa vya watu kuumia katika mkurupuko wa kupanga foleni vituo vilipofunguliwa viliripotiwa.
Watu walianza kupanga foleni nje ya vituo mapema
Katika moja kati ya vituo vinne nchini humo, maafisa wa IEBC walikuwa wamesema kwamba hakuna huduma nzuri ya mtandao maana kwamba wasimamizi wa uchaguzi katika vituo hivyo watahitaji kusafiri hadi ameneo yenye huduma nzuri ya simu kutuma matokeo kikamilifu.
Kumekuwa pia na taarifa kwmaba mwanamume mmoja ameuawa katika makabiliano kati ya wafuasi wa wagombea wawili katika kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya.
Lakini kulikuwa na kisa cha kutia moyo pale mwanamke mmoja alipojifunzua mtoto msichana alipokuwa kwenye foleni akijiandaa kupiga kura Pokot Magharibi.
Pauline Chemanang alisema kujifungua kwake ni baraka na akampa mtoto wake jina Kura, kwa mujibu wa kituo kimoja cha redio.
Maafisa wa uchaguzi wanaendelea kuhesabu kura hapo jana
"Kwa wapinzani wangu, kama nilivyosema mara nyingi awali, ikitokea kwamba washindwe, basi hebu tukubali uamuzi wa wananchi. Nina nia, mwenyewe, kukubali nia ya wananchi," amesema.
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipiga kura yake katika mtaa wa Kibera, Nairobi.
Akiongea nje ya kituo hicho, aliwahimiza wafuasi wake: "Hebu tujitokeze kwa wingi na tupige kura."
Kabla ya siku ya uchaguzi, meneja wa masuala ya teknolojia katika IEBC Chris Msando aliuawa na watu wasiojulikana.
Kulikuwepo na madai ya kwamba huenda kukawa na wizi wa kura na pia katika baadhi ya maeneo taarifa za kueneza kwa karatasi zenye ujumbe wa chuki zilizagaa.
Siku chache kabla ya uchaguzi, Wakenya wengi walikuwa wakinunua chakula na maji na kujihifadhia wakihofia hali baada ya uchaguzi.
Polisi pia walifanya mipango ya kushughulikia dharura iwapo ghasia zingetokea.


No comments