WAZIRI MHAGAMA AAGIZA KIPANDE CHA BARABARA YA KIWANGWA-MABOHELO KUKAMILIKA IFIKAPO MWISHONI MWA DESEMBA 2016
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Walemavu Mhe.Jenista Mhagama
Na Daudi Manongi
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Walemavu Mhe.Jenista Mhagama amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.
Majid Mwanga kuhakikisha ana tatua mgogoro wa ujenzi wa barabara ya
Kiwangwa-Mabohelo yenye urefu wa kilomita 15 na kumalizika mwishoni mwa
mwezi huu.
Ameyasema
hayo jana Wilayani wakati alipotembelea miradi inayotekelezwa na
Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na Bagamoyo kwa ufadhili wa Programu
ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini(MIVARF) inayosimamiwa na chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
“Serikali
ya Awamu ya Tano ina lengo kubwa la kuwasaidia wananchi hususani
wakulima ili wafikiwe na miundombinu ili kupambana na umaskini na
kuboresha masuala ya masoko yao na hivyo kuwaongezea kipato”, Alisema
Mhagama.
Aidha
Mhe. Mhagama alisema kuwa asili ya miradi ya ufadhili wa Programu ya
Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini
(MIVARF) iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu haina fidia hivyo
anashangaa kuona ni kwanini ujenzi vipande hivyo vitatu vya barabara
vinachelewa kukamilika hadi kufikia leo.
Ameongeza
kuwa pesa za kumalizia mradi huo zipo na kusema kuwa tatizo kubwa
lililopo ni kukosekana kwa mawasiliano kati ya Halmshauri za Bagamoyo na
Chalinze na kuwaagiza Viongozi wa Halmashauri hizo chini na kumaliza
mgogoro huu mara moja ili wananchi wafanikishe lengo kuu la mradi huo
ambao ni umwagiliaji.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe.Ridhiwani Kikwete alisema
kuwa tatizo kubwa linalofanya mradi huo kutokamilika ni kutoshirikishwa
kwa wananchi na kuitaka halmashauri ya Bagamoyo kukaa pamoja na wao
ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Bw.Majid Hemed Mwanga aliahidi kulipatia
ufumbuzi tatizo la mgogoro huo ndani ya muda alioagizwa kwa
kuwashirikisha madiwani wote.

No comments