Naibu Waziri wa Afya akagua vituo vya afya wilaya ya kati
Na Mwashungi Tahir, Maelezo Zanzibar
NAIBU
Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman, amewataka wafanyakazi wa vituo
vya afya nchini kutumia lugha nzuri wakati wanapowahudumia wagonjwa ili
kuwajengea imani na mapenzi kwao.
Aidha, amewasisitiza kuwa na huruma wakielewa wagonjwa ni binadamu wanaohitaji kufarijiwa wanapokuwa wanaumwa.
Wito
huo ameutoa leo Disemba 21, 2016 katika ziara aliyoifanya kukagua
vituo vya afya vilivyoko wilaya ya Kati na kuzungumza na wafanyakazi wa
vituo hivyo.
Naibu
Waziri huyo amesema, mbali ya dawa zinazotolewa kwa wagonjwa, lakini
lugha nzuri na unyenyekevu wa madaktari na wauguzi katika kuwahudumia,
ni tabibu mzuri kwao.
Amefahamisha
kuwa, lugha nzuri, imani na upendo, ndio njia pekee inayoweza
kuwafariji wagonjwa na kuwahamasisha kuvitumia vituo vya afya kila
wanapopatwa na maradhi.
Aidha,
amewahimiza wafanyakazi wa vituo hivyo kuongeza ushirikiano kazini kati
yao wenyewe pamoja na viongozi wao ili kuleta ufanisi katika utendaji
wa kazi.
Akiwa
katika ziara hiyo, amepata fursa ya kufahamu changamoto mbalimbali
zinazovikabili vituo vilivyomo wilayani humo, ikiwemo ukosefu wa
vitendea kazi, uhaba wa madaktari.
Katika kituo cha Bambi, Naibu Waziri huyo alibaini tatizo la kuvuja kwa paa pamoja na ukosefu wa maji safi na salama.
Hata hivyo, ameeleza kufurahishwa na moyo wa kujituma walionao wafanyakazi licha ya kukabiliwa na mazingira magumu.
Kwa
upande wake, Mkuu wa wilaya ya Kati Mashavu Sukwa Said, ameuomba
uongozi wa Wizara ya Afya kupunguza tabia ya kuwahamisha madaktari mara
kwa mara, akisema kufanya hivyo ni usumbufu kwao pamoja na wagonjwa.
Mkurugenzi
Kinga Dk. Fadhil Mohammed Abdalla, amesema wizara inatambua kuwepo na
uhaba wa wafanyakazi katika vituo mbalimbali lakini akasema tayari
tatizo hilo linashughulikiwa.
Vituo vya afya vilivyotembelewa ni Uzini, Bambi na Mwera.
No comments