Serikalini yatahadharisha wananchi Arusha na baa la njaa

Wito umetolewa kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuchukua tahadharisha , kuanza kuchukua juu ya tishio la baa la njaa kwa kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha.

Tahadhari hiyo imetolewa na  Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Gabriel Daqaro
alisema  uhaba wa mvua za vuli ulioikumba Arusha imefanya wakulima
kutopata mavuno mazuri na kuleta dalili tosha za wilaya zake kukumbwa
na njaa.

Kufuatia hilo aliwataka wananchi wa mkoa wa Arusha kupunguza matumizi
mabaya ya chakula walichonacho ikiwemo kusaza, na badala yake
wajiwekee akiba sambamba na wale wasio nacho wanunue wahifadhi.

"Kama mnavyoona upungufu wa mvua kwa msimu huu  ni dalili tosha za
uhaba wa chakula baadae ukizingatia wakulima wengi Arusha wanategemea
kilimo cha mvua  hivyo basi wajitahidi kila mtu kununua chakula mapema
hasa kipindi hiki ambacho bado hakijapanda bei maana hali itakuwa
mbaya zaidi,"alisema.

"Nasema hivyo kwa sababu kwa sasa chakula bado kiko sokoni kwa bei
nzuri, lakini kipindi cha ukame kukifikia mazao hayo yatakuwa ghali
sana hivyo kuwafanya wasiomudu gharama kuanza kulia kulia,"alisema

Mbali na hilo Daqaro aliwataka maafisa kilimo kutembelea wakulima
kuanza kutoa elimu juu ya mazao yanayostahimili ukame lakini pia ya
mda mfupi ili angalau wakulima waache kilimo cha mazoea badala yake
walime kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa pia kwa ubunifu wa mazao
ya kulima

"Nasema hivyo kwa sababu nimegundua wakulima wengi wakiona mvua bila
kujua ni kidogo au ya kutosha wanalima mazao waliyozoea, badala ya
yanayostahimili hali ya hewa, lakini pia maafisa ugani wawaelimishe
wakulima wale walio karibu na miundombinu ya maji wajikite kwenye
kilimo cha umwagiliaji"

Kwa Wilaya ya Monduli inayojishughulisha zaidi na ufugaji, Mkuu wa
Wilaya hiyo, Idd Hassan Kimanta aliwataka wananchi wake kupanda nyasi
za kutosha kwa ajili ya malisho.

"Mvua za mwaka huu zimekuwa kidogo sana hivyo kutokana na wilaya yangu
kujishughulisha zaidi na ufugaji, niwatake tu watumie mvua hizi kidogo
kupanda nyasi kwa ajili ya malisho ingali ardhi ina unyevu nyavu hasa
sehemu za Selela, mto wa Mbu, Engaruka, na makuyuni ambapo manyunyu
bado inapita,"alisema.

"Lakini pia watumie  mifugo yao kibiashara badala ya ufahari kwa kuuza
kidogo wanunue chakula cha kuhifadhi tena msimu huu wa sikukuu ambao
mifugo ni bei juu, kuliko kusubiri hadi ikumbukwe na njaa na
kukondeana,"alisema.

Akizungumzia tahadhari hiyo, mmoja wa wakulima Kata ya Terrat Wilaya
ya Arusha, Sailevu Mollel  alisema  kilimo cha mwaka huu kimekuwa
kigumu, kutokana na serikali kutokuchukua tahadhari mapema ya
kutangaza mabadiliko hayo ya hali ya hewa juu ya uhaba wa mvua za
vuli, hivyo kupanda mazao yao ambayo yameishia kukauka na kuwa hasara
kwao.

"Tunasikia wako maafisa ugani kila eneo wanatakiwa kuja mapema kusema
jambo hili, lakini hatuwaoni hadi hasara itokee ndio serikali kuu waje
kusema wakati tumeshataabika, lakini pia pembejeo za kilimo wala
mashamba darasa hakuna vijijini ambako ndio sehemu zenye mashamba,
hivi tunaweza kweli kuepuka baa la njaa hasa sisi wakulima
tunaotegemea kilimo kwa asilimia 100,"alisema Sailevu





No comments