WATATU WAFA MKOANI MANYARA
![]() |
Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Chelestino Mofuga akizungumza na wananchi wa bonde la Yaeda Chini, baada ya kutokea mauaji ya watu watatu kuchomwa moto
|
Na.Mwandishi wetu Manyara.
Watu watatu wameuawa kwenye bonde la Yaeda Chini katika matukio tofauti, ikiwemo wawili kuchomwa moto na mwanamke mjamzito kuchomwa mkuki na kufa.
Mkuu wa wilaya hiyo Chelestino Mofuga akizungumza jana alisema matukio hayo yalitokea juzi kwenye vijiji vya Dumanga na Mongo wa mono, kwenye bonde la Yaeda Chini.
Mofuga alisema katika tukio la kwanza watu watatu waliodaiwa kuwa majambazi walipora pikipiki na wakati wanakimbia mmoja aliyejulikana kwa makafo Elia alishindwa kukimbia akakamatwa na wananchi wenye hasira.
Alisema baada ya mafuta ya pikipiki kuisha ,aliuawa na kuchomwa moto na kuteketea hadi kuwa majivu.
Alisema tukio la pili Martin Boay (25) alimchoma mkuki mwanamke mjamzito Elizabeth Elias (35) na kufariki na fanaka wananchi wenye hasira waliamua kumfunga mikono na miguu na kumtupa kwenye moto akaungua hadi kuwa majivu.
"Hadi hivi sasa bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa matukio hayo matatu ili kuhakikisha mambo hayo ya kujichukulia sheria mkononi yanakomeshwa," alisema Mofuga.
Alisema kamati ya ulinzi na usalama imekemea vikali wananchi tabia ya kuchukua hatua za kisheria mikononi.
Pia, mkuu huyo wilaya amemuagiza mkuu wa polisi wa wilaya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya walihusika na matukio hayo ili iwe fundisho kwa wengine.
"Bonde la Yaeda chini lina historia ya matukio ya uhalifu hasa mauaji, ujangili wa nyara za serikali na wizi wa mifugo, tunaanzisha harambee kwa kuhamasisha wananchi na wadau wengine ili kujenga kituo cha polisi katika bonde hilo," alisema.
Alisema Kituo cha polisi kinatarajiwa kugharimu sh135 milioni na nyumba sita zitakazojengwa kwenye jengo moja kwa gharama ya sh150 milioni.
Alisema ujenzi wa kituo na nyumba za familia 12 utagharimu sh435 milioni na unatakiwa kuanza mara moja.
Alisema ameanza harakati za kuomba wadau, wananchi na serikali kuchangia ujenzi huo ili kutafuta amani ya kudumu katika bonde la Yaeda chini.
Mkazi wa eneo hilo Stephen Songay alipongeza jitihada za mkuu huyo wa wilaya za kujenga kituo cha polisi ili kukomesha matukio ya mauaji kwenye eneo hilo.
"Kituo cha polisi Haydom au Dongobesh ni mbali zaidi ya kilometa 80 hivyo jamii ya bonde la Yaeda Chini kunapaswa kuwe na kituo cha polisi hapa karibu," alisema Songay.

No comments