Wadau wa Maendeleo watakiwa kuchangia ujenzi wa kituo cha Polisi
Na.Mwandishi wetu Manyara.
Wadau wa maendeleo Mji mdogo wa Haydom waombwa kuchangia ujenzi wa kituo cha pilisi Bonde la Yaeda Chini.
Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya ya Mbulu mkoa wa Manyara Chelestino Mofuga hivi karibuni aliposhiriki kwenye ibada na wananchi wa eneo hilo katika kanisa la KKKT usharika wa Haydom.
Chelestino alisema kuwa njia ya kudumu ya kudhibiti matukio ya ujangili wa nyara za serikali, wizi wa mifugo na mauaji ya binadamu ni ujenzi wa kituo cha polisi ambao unakisiwa kugharimu shilingi 135 milioni na nyumba mbili zitakazoishi familia 12 ambazo nazo zitagharimu 300 milioni
"Kupitia nafasi hii nawaomba mchangie ujenzi wa kituo cha polisi cha Yaeda Chini ili kudhibiti uhalifu unaojitokeza katika eneo hilo," alisema Mofuga.
Alisema kuwa wananchi wamehamasika na kuanza kuchangia ujenzi wa kituo cha polisi na nyumba za askari ambapo nusu ya gharama zinatarajiwa kuombwa kwa wadau mbalimbali na nyingine serikali itagharamia.
"Natarajia zoezi hili litafanyika kwa ufanisi mkubwa na kituo cha polisi kitajengwa ili kuhakikisha usalama na amani ya kudumu inakuwepo," alisema Mofuga.
Mkazi wa eneo la bonde la Yaeda Chini John Aron alipongeza juhudi za mkuu huyo wa wilaya katika kuhakikisha kituo cha polisi kinajengwa.
"Kuwaita polisi kutoka Haydom au Dongobesh ni mbali zaidi hivyo ujenzi wake hapa utachochea hali ya usalama kuwa ya kutosha," alisema Aron.
Richard Aloyce alisema ni bora ujenzi huo ufanyike kuliko baadhi ya wanasiasa waliokuwa na wazo la kubadilisha jengo la mifugo la kata kubadilishwa matumizi kuwa kituo cha polisi.
No comments