Busara za Wazee zakumbukwa kuelekea Tanzania ya Viwanda
Jamii imetakiwa kutambua umuhimu wa wazee na kuwatumia kwa ushauri mbalimbali hasa katika kuelekea uchumi wa viwanda katika serikali ya awamu ya tano kutokana na uzoefu walionao tangu wakiwa nguvu kazi ya Taifa.
Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya wazee duniani jiji la Arusha Afisa maendeleo ya jamii Janeth Masasi ambaye alikuwa anamuwakilisha mkurugenzi wa jiji kama mgeni rasmi amesema wazee ndiyo hazina hivyo tunatakiwa tuwatumie katika ushauri ili kuinua uchumi wa nchi.
Katika maadhimisho hayo ambayo kilele chake ni tarehe Mosi Octoba 2017 yameanza katika jiji hilo kwenye viwanja vya Makumbusho ambapo wazee watapata fursa ya kupimwa afya zao bure na madaktari ambao ni wataalamu wa magonjwa ya wazee.
Naye Dokta Sadick Temu ambaye anasimamia zoezi hilo amesema kuwa magonjwa yatakayopimwa kwa siku hizo mbili ni Kisukari,Presha,Macho Pamoja na uzito kwakuwa ndiyo magonjwa yanayowasumbua zaidi wazee.
Akizungumza Afisa ustawi wa Jamii Martha George amesema kuwa wameamua kufanya hivyo ili kuhakikisha kila mzee anafikiwa hivyo kwa siku hizo mbili wanategemea kupima afya za wazee zaidi ya 1000.
Maadhimisho ya siku wazee duniani huadhimishwa kila mwaka taehe mosi Octoba ambapo mwaka huu kitaifa yatafanyika katika viwanja vya Nyerere Square Mkoani Dodoma na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Raisi mstafu wa awamu ya Pili Mh Ali Hassani Mwinyi na kauli mbiu ni “KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA TUTHAMINI MCHANGO ,UZOEFU,NA USHIRIKI WA WAZEE KWA MAENDELEO YA TAIFA”
Maadhimisho ya siku ya wazee duniani ni moja kati ya jitihada za baraza kuu la umoja wa mataifa (UN)katika kutambua na kuhamasisha jamii kulinda na kutetea haki za wazee duniani Kote.
Hata hivyo umoja wa mataifa unatenga siku hiyo kwa lengo la kutafakari hali ya maisha ya wazee na changamoto zinazowakabili wazee na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na kuwafanya waishi maisha ya heshima,hadhi na kuthamini utu wao
No comments