LEKULE:WEKENI KUMBUKUMBU KATIKA JAMII
Na mwandishi wetu.Arumeru.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha Lekule Laizer, amewataka vijana wa jamii ya kifugaji wa kimasai wa kata ya Majengo Wilayani Arumeru waliovuka rika na kuwa wazee, waache kumbukumbu yao kwa kujenga zahanati itakayokuwa inatoa huduma za afya kwenye eneo hilo.
Laizer aliyasema hayo jana kwenye kijiji cha Engatani kata ya Majengo katika sherehe za kuvuka rika kwa vijana kusimikwa kuwa wazee.
Alisema vijana hao hivi sasa wamevuka rika na kuwa wazee hivyo ili waweze kuacha kumbukumbu nzuri ya rika lao wanapaswa kuanzisha ujenzi wa zahanati ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa matibabu pindi jamii ikiugua.
Alisema wanapaswa kufanya jambo la maana kwa kujenga zahanati na yeye akiwa mdau wa maendeleo atawaunga mkono endapo wataandaa harambee.
"Mnapaswa kutambua kuwa baada ya kufanya jambo la kumbukumbu kwa kujenga zahanati kwenye hatua ya linta serikali itawaunga mkono kwenye kupaua na kumalizia jengo hilo," alisema Laizer.
Aliwataka vijana hao kutambua kuwa wameacha ujana na kuingia kwenye uzee, hatua ambayo ni kubwa mno na ya kuheshimiwa katika jamii hiyo.
"Katika kundi la wazee ndipo kunatakiwa kuwe na hekima na busara zaidi na wazee wakubwa wanawategemea mno kwa kuendeleza maendeleo na mambo ya mila na utamaduni wa jamii hii," alisema Laizer.
Mmoja kati ya vijana waliovuka rika, Ephrahem Mollel akisoma risala alisema wamefanikiwa kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za ujasiriamali ikiwemo ufugaji, kilimo, biashara na uchimbaji madini, hivyo kupunguza ufukara katika jamii hiyo
Mollel alisema wamefanikiwa kutoa michango ya hali na mali kwa kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo katika jamii ikiwemo shule tatu za msingi kwenye kata hiyo na moja ya sekondari ambayo ipo katika ujenzi na inatarajiwa kufunguliwa mwakani.
Alisema wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa elimu kwani asilimia 90 ya vijana hao 200 waliovuka rika hawajui kusoma wala kuandika hali inayosababisha wakose ajira.
Alisema nishati ya umeme imewazunguka kila eneo na wao walichangia fedha za gharama za kuvuta nguzo na nyaya ila hadi hivi sasa wanaambiwa wasubiri awamu ijayo ya Rea ili wapatiwe.
"Pamoja na hayo hatuna josho la mifugo ambayo ndiyo shughuli yetu ya kiuchumi, barabara zetu ni mbovu na pia hatuna mabwawa ya kutosha ya kuvunia maji ya mvua kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo," alisema Mollel

No comments