Mkuu  wa Trafiki apata ajali

Mkuu  wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani  Pwani  (SSP) Abdi Issango amelazwa kwenye Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi Kibaha Mkoani Pwani baada ya kupata ajali.

Kamanda huyo amepata  ajali  Septemba 16, saa kumi jioni Kijiji cha Kibiki Wilaya ya kipolisi ya Chalinze mkoani humo akiwa na familia yake ambapo  baba yake mzazi alifariki papohapo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani Jonathan Shanna amemtaja  marehemu kwamba anaitwa Hamis Issango, huku akisema  mama yake mzazi alijeruhiwa vibaya huku ndugu yake mmoja akipoteza maisha.

"Ajali  imesababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi  wanne akiwemo  Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani na aliyefariki ni baba yake’’alisema

Pia amesema  majeruhi wengine ni mdogo wake ambaye ni mwanafunzi hao wote wamelazwa kwenye Hospital ya Tumbi.

Amesema kamanda huyo alikuwa akisafiri na familia yake hiyo kutokea  Singida kuelekea Kibaha na waliligonga kwa nyuma lori  lillokuwa limeharibika barabarani.

Kamanda shanna amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori  aliyeshindwa kuweka alama za kuashiria  gari lake ni bovu alilokuwa ameliegesha  pembezoni mwa barabara.

 Kamanda Shanna amesema dereva wa lori hilo na utingo wake walikimbia polisi wanaendelea  kuwatafuta.

  Chanzo: mwananchi

No comments