Wasanii wa filamu wa china kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania

WATANZANIA wametakiwa kuendeleza ukaribu kwa wageni na kuhifadhi vivutio vya utalii ili kushawishi wageni wengi kuja nchini kwa utalii ambao una nafasi kubwa ya kuitangaza Tanzania ulimwenguni.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)  Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, katika hafla ya kuwaaga wasanii maarufu wa filamu kutoka China waliokuja nchini kwa shughuli za kisanii na kuangalia vivutio vya utalii kuwa Tanzania ni tajiri kwa vivutio vyingi vya utalii.

“Bado nchi yetu inajipambanua kwa amani duniani, wageni wengi wanavutiwa kuja kufanya shughuli mbalimbali za kisanii na kujifunza utamaduni wetu kutokana na sifa kubwa ya amani na utulivu, tuzilinde tunu hizi ili waje wengi zaidi,” alisema.

Jaji Mihiayo alisema  kwa upande wa utalii Tanzania imenufaika kupata wageni hao ambao miongoni mwao ni wasanii maarufu katika nchi yenye watu zaidi ya bilioni 1.2.

 “Siyo  Wachina wote wanaijua Tanzania lakini kupitia mabalozi hawa tutaendelea kupokea wageni wengi kutoka huko,” aliongeza Jaji Mihayo, na kuwaomba wasanii hao kuwa mabalozi wazuri watakaporudi nchini kwao.

Katika hafla hiyo iliyofanyika usiku wa kuamkia jana kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini hapa, kulikuwepo na wasanii maarufu saba walioambatana na wasaidizi wao ambao kwa pamoja walikuwa 150.

Jaji Mihayo alisema wasanii hao walikuwepo Tanzania kwa siku 15 kwa shughuli ya uigizaji kwa ajili ya mfululizo wa filamu kupitia Hunan Television. Maeneo waliyotembelea ni Ngorongoro, Serengeti, Visiwa vya Pemba na Dar es Salaam.

Msanii maarufu nchini China, Li-Yu anayeigiza nafasi ya mpambanaji dhidi ya rushwa katika tamthilia ya ‘In the name of the people’ inayoendelea sasa nchini humo kupitia Hunan Television, alisema wiki mbili walizokaa Tanzania hawatazisahau kutokana na aina ya watu waliokutana nao wenye upendo na huruma.

“Tumekutana na mazingira murua, watu murua katika nchi nzuri yenye kuvutia, tumefurahia kila hatua tuliyopiga na sekunde iliyopita. Kitu ambacho sitakisahau nikiondoka katika ardhi hii ni umuhimu wa kutunza wanyamapori, Tanzania ina wanyama wazuri wa kuvutia sijawahi kuona maishani mwangu.

“Nitabeba jukumu la kuhifadhi mazingira na wanyamapori, kwa sababu nimebaini ni kitu kinachoburudisha macho. Tumefika visiwa vya Pemba hakika kuna fukwe nzuri za kupumzisha akili baada ya kazi nzito, hakika tumechagua eneo zuri la kuchukua vipande vya filamu tutakayowaonyesha Wachina wenzetu,” alisema Bwana Li-Yu.
 “Tanzania ni mahali panapovutia macho kama uchawi na China ni nchi yenye watu wengi wenye utamaduni mbalimbali ambao asilimia kubwa wanapenda kutembelea maeneo mbalimbali duniani,” Alisema Jaji Mihayo.

Alisema muunganiko huu utasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini kama Mamlaka ya Utalii China (CNTA) ilivyoorodhesha mataifa saba muhimu kwa utalii duniani na Tanzania ikawemo basi tutahakikisha hatuwaangushi.
Wakati hafla hiyo, TTB kupitia Mwenyekiti wake wa Bodi walitoa  zawadi za shuka za Kimaasai kwa wasanii hao kama kumbukumbu kwao.

 “Kwa utamaduni wa Kiswahili unapotembelewa na mgeni unamweleza kuwa ikiwa kuna lolote tulilowakosea naombeni mliache hapahapa na tutalishughulikia ipasavyo ili mkija siku nyingine mtakuta limerekebishwa. Nanyi tunaomba mfanye hivyo, mabaya yaacheni hapahapa ondokeni na mazuri tu.” Alisema.

Katika watu maarufu saba waliotajwa katika ujumbe huo kuna wasanii wa filamu, mshindi wa mashindano ya Olympic na mshindi wa mashindano ya urembo China.

Vipande vya filamu walivyoigiza katika maeneo mbalimbali ya kitalii nchini vitatumika katika mfululizo wa tamthilia inayoonyeshwa Hunan TV, ambayo ina watazamaji zaidi ya milioni 800 katika nchi hiyo yenye watu wanaofikia bilioni 1.2.

No comments