MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA RAIS WA SHIRIKA LA DATANG KUTOKA CHINA
Shirika la Datang Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China lina mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano nchini kwa ushirikiano na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Rais
wa Shirika hilo Yuan Yong ametoa kauli hiyo 1-Mar-2017 baada ya kukutana
na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.
Yuan
Yong amemweleza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Serikali ya
China pia ina mpango wa kuikopesha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kiasi
cha shilingi bilioni 600 ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na kupanua
mtandao wa mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini hasa vijijini.
Rais
huyo amesema lengo la mkakati huo ni kuifanya TTCL kuwa Kampuni bora
inayotoa huduma za mawasiliano kwa njia ya kisasa kuliko kampuni yeyote
katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Amesema
kuwa mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China ndio yamepelekea
shirika hilo kuweka mikakati ya kuja kuwekeza nchini katika sekta ya
mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wa Tanzania wanapata huduma bora za
mawasiliano mijini na vijijini kwa njia ya kisasa bila usumbufu wowote.
Kwa
upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia
Suluhu Hassan ameonyesha kufurahishwa na mikakati hiyo na kusisitiza
kuwa serikali ipo tayari kwa uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya manufaa
ya wananchi wa pande hizo Mbili.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema anaimani kubwa kuwa uwekezaji
huo ukikamilika utaiwezesha (TTCL) kufanya kazi kwa ubora wa hali ya juu
kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Makamu
wa Rais amesema serikali ya awamu ya Tano imedhamiria kuelekea katika
uchumi wa viwanda kwa kishindo hali ambayo itasaidia taifa kuongeza pato
lake la taifa pamoja na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi kupitia
viwanda ambazo vitajengwa nchini.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amepongeza mpango wa Shirika hilo
la Mawasiliano la Serikali ya China wa kutoa mafunzo mbalimbali kwa
wafanyakazi wa TTCL ikiwemo ujenzi wa Kituo Kikubwa cha Utafiti wa
Mawasiliano nchini hatua ambayo itasaidia kuimarisha utendaji kazi kwa
wafanyakazi wa TTCL ili waweze kuendana na teknolojia ya kisasa ya
mawasiliano Duniani kupitia tafiti zitakazofanywa nchini.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu- Dar es Salaam.
1-Mar-2017.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan akizungumza
na Rais wa Shirika la Datang Telecom International Technology Company
Limited la Serikali ya China Bw.Yuan Yong (kulia) pamoja na ujumbe wake,
Ikulu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
10:Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu
Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Shirika la Datang
Telecom International Technology Company Limited la Serikali ya China
Bw.Yuan Yong na ujumbe wake mara baada ya kupokea taarifa ya mpango wa
serikali ya China wa kuikopesha TTCL ili kuipa uwezo wa kiteknolojia na
kupanua mtandao wa mawasiliano vijijini na mijini pamoja na kujenga
kiwanda cha kutengeneza vifaa vya mawasiliano hapa Tanzania. (Picha na
Ofisi ya Makamu wa Rais).



No comments