BUNDUKI KUMI ZIKIWEMO SMG SITA RISASI 59 ZAPATIKANA ARUSHA
Silaha mbalimbali zikiwemo SMG 6 pamoja na risasi 59
zilizopatikana katika operesheni iliyofanyika katika wilaya ya
Ngorongoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles Mkumbo
akionyesha silaha mbalimbali zilizopatikana katika operesheni
iliyofanyika wilayani Ngorongoro iliyofanyika wiki mbili zilizopita.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles
Mkumbo akionesha waandishi wa habari baadhi ya silaha zilizopatikana
katika operesheni iliyofanyika wilayani Ngorongoro.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha akiwaonesha waandishi wa habari
moja ya silaha ya kivita aina ya Chinese 56 Sub Machine Gun (SMG)
iliyopatikana kwenye operesheni iliyofanyika wilayani Ngorongoro.
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi
Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupata jumla ya
bunduki kumi za aina nne tofauti zikiwemo Sub-Machine Gun sita baada ya
operesheni ya wiki mbili iliyoanza tarehe 15.02.2017 katika wilaya ya
Ngorongoro.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo asubuhi,
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema
silaha hizo zilipatikana katika vijiji vya Olorieni Magaiduru, Oldonyosambu na
Sale vilivyopo katika tarafa za Loliondo na Sale.
Alisema mafanikio hayo yalitokana na taarifa fiche ambazo
zilibainisha kwamba kuna baadhi ya watu wanamiliki silaha za kivita hivyo
mahojiano makali baina ya askari wa Jeshi la Polisi na Viongozi wa Kimila na
kuwataka wasalimishe silaha popote pale ambapo walikuwa wanaamini kwamba silaha
hizo zitawafikia Jeshi la Polisi.
Akibainisha vijiji ambavyo silaha hizo zilipatikana kuwa ni
Olorieni Magaiduru zilipatikana silaha aina ya Chinese 56 SMG moja yenye namba
MT. 70B 1 2730021 na risasi 21 pamoja na silaha aina ya Semi Automatic Rifle
(S.A.R) yenye namba KN 250374 ikiwa na risasi nne.
Katika kijiji cha Oldonyasambu ilipatikana silaha aina ya
Mark IV yenye namba ZKK 5602 pamoja na silaha nne aina ya Chinese 56
Sub-Machine Gun (SMG) zikiwa na risasi 19. Silaha hizo nne ni Chinese 56 SMG
yenye namba RT 7663, bunduki ya pili namba yake ni 563631144 na bunduki mbili
nyingine hazikuwa na namba.
Kamanda Mkumbo alisema katika kijiji cha Sale silaha aina ya
Chinese 56 SMG yenye namba 89020539 ikiwa na risasi 15 kwenye magazine
ilipatikana pamoja na silaha nyingine mbili tofauti ambazo ni S.A.R yenye namba
25032534 na Mark III yenye namba 263126.
Aidha kamanda Mkumbo aliwataka wananchi wanaomiliki silaha za
moto kinyume cha sheria wazisalimishe mara moja kwenye ofisi za mitaa, vijiji na
hata vituo vya Polisi vyovyote vilichopo karibu huku akitoa onyo kwa wale ambao
watakaidi na wakikutwa nazo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. Alisema
Operesheni hiyo ni endelevu na itakuwa katika maeneo tofauti ya mkoa huu na si wilaya
ya Ngorongoro pekee.
No comments