WANANDOA KUACHANA KWA MKATABA MAALUM BILA KWENDA MAHAKAMANI
NA BASHIR YAKUB -
Zipo namna nyingi za kuachana kisheria kwa wanandoa ambao wanadhani sasa hawawezi kuendelea. Wengi wetu tunajua zile za kupitia mahakamani. Zile ni sahihi lakini upo uwezekano pia wa kuachana kwa mkataba maalum bila kuhitaji kwenda mahakamani.
Aidha yafaa ifahamike kuwa Kuachana katika ndoa na kuamua kuishi nje ya ndoa ni jambo la kawaida. Kisheria si dhambi mwanandoa yeyote kuona kuwa sasa hawezi kuendelea kuwa katika ndoa. Ni kwasababu hii hata sheria ikatambua uwezekano wa watu kuachana na halikadhalika ikaweka utaratibu maalum kwa walio tayari kwa hilo.
Tofauti na kuachana kwa mkataba namna nyingine ni kwa njia ya talaka mahakamani na kwa njia ya kutengana mahakamani ambazo nazo tutaziona hapa chini kabla ya kutizama ile ya mkataba.
1.KUACHANA KWA TALAKA.
Kifungu cha 99 cha Sheria ya ndoa kinaongelea talaka. Maombi ya talaka hupelekwa na yule anayedhani hawezi kuendelea na ndoa kutokana na sababu anazoamini kuwa ndoa hiyo haiwezi kuendelea. Mahakama huzisikiliza pande zote mbili na kuja na maamuzi.
Kifungu cha 107( 2 ) cha sheria ya ndoa kinazitaja sababu ambazo zote au mojawapo ikithibitishwa ni ushahidi kuwa ndoa hiyo haiwezi kuendelea. Baadhi ni ukatili, zinaa, kutelekeza, kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka mitano, na nyingine nyingi.
Talaka huombwa mahakamani na hivyo maombi yake hupelekwa mahakamani.
2. KUTENGANA MAHAKAMANI BILA TALAKA.
Hatua hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 99 cha sheria ya ndoa. Mnatengana kwa muda fulani lakini bila talaka. Talaka ni kutengana milele wakati hii ni kutengana kwa muda. Njia hii nayo muombaji hutakiwa kwenda mahakamani na kufungua maombi.
Wahusika wote wataitwa na kila mmoja atajieleza na baadae mahakama itatoa maamuzi. Njia hizi zote mbili mwombaji hutakiwa kupitia mahakamani isipokuwa hii ya mkataba ambayo itaelezwa hapa chini.
3. KUACHANA KWA MKATABA MAALUM.
Kifungu cha 67 cha sheria ya ndoa kinasema kuwa wanandoa wanaweza kwa njia ya maandishi ambayo yatakuwa yamesainiwa na wote wawili kuamua kuishi tofauti/nje ya ndoa. Kwahiyo utaona hapa kuwa unachotakiwa kufanya ni kukubaliana na mwanandoa mwenzako kwamba sasa naona mambo hayaendi na hivyo ni bora kila mtu aishi maisha yake.
Akikubali basi mtakaa chini mtaandikishana kisheria kabisa na kila mtu ataendelea na maisha yake. Isipokuwa ni lazima mnapoamua kutumia njia hii hakikisha katika maandiko yenu viwemo vipengele vinavyohusu matunzo ya watoto/mtoto kwa maslahi mapana kabisa, muafaka na hatima kuhusu mali mlizonazo, pia matunzo au vinginevyo kwa mmoja kati ya wanandoa kama hilo litakuwa ni la lazima.
Kwahiyo haya ni maandiko na ni mkataba sawa na mikataba mingine ya kisheria. Faida ya njia hii ni kuwa ni nyepesi, haitumii mda mwingi, haina gharama kubwa na inatekelezeka kwa urahisi.
No comments