HOJA YA HAJA: NINAVYOIONA CCM YA SASA
Nianze
kwa kuitakia heri ya kumbukizi ya miaka 40 ya kuzaliwa kwa Chama Cha
Mapinduzi, chama kinachoendelea kushika dola ya Tanzania toka kiasisiwe
mwaka 1977 ambalo ni zao la vyama vya TANU na ASP.
Misingi
mizuri iliyojengwa na waasisi wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius
Nyerere (Tanganyika- Bara) na Abeid Amani Karume (Zanzibar - Visiwani)
imesababisha Wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu kuishi kwa amani na
utulivu huku wakifanya mambo yao kwa uhuru bila ya kuingiliwa na mtu
yeyote Yule.
Tofauti
na mataifa mengine Watanzania wako huru zaidi kwenda kokote kule ndani
ya nchi na hata kuishi au kufanya kazi ama biashara bila ya bughudha
yoyote endapo taratibu na sheria zitazingatiwa vyema.
Hali
hii ni tofauti na nchi nyingine zikiwemo za jirani kama vile Kenya ,
Kenya Rwanda, Burundi, Kongo na hata Uganda ambapo ukabila umetalaki
kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa lakini kwa Tanzania hakuna ubaguzi wa
rangi,dini wala kabila.
Hiyo
inatokana na uongozi imara, sera safi, upendo na kila aina ya ubora
uliotukuka ndani yake kwa jamii ya kitanzania. Jambo linaloendelea kutia
faraja ni kuwa tangu ianzishwe CCM imeendelea kuwa ni chama
kinachotawala na kuongoza nchi. Na siri yote ya mafanikio hayo ni
kutokana na kuwa nguzo imara ambazo ni Wanachama, Ilani ya chama, na
Viongozi wake.
Wanachama
wake ambao ndio mtaji wa chama wapatao zaidi ya milioni nne na nusu na
mashabiki wapatao ama zaidi ya milioni 10. CCM ni chama kisichozingatia
uwepo au hata harufu ya ubaguzi wa rangi, kabila au dini ya mtu.
Hatua
hio imewafanya Watanzania wengi kuanzia vijana kwa wazee, wake kwa
wanaume kujivunia kuwa wanachama makini wa chama chenye mtazamo chanya
wa kuwavusha kwenye neema. Ili kuhakikisha CCM inapata makada wa aina
tofauti bila ya kujali umri, jinsia ilianzisha jumuiya za wazazi,
wanawake (UWT) na vijana (UVCCM) ambazo ni viungo muhimu vya chama
katika kuwaweka watu wote pamoja na karibu na hivyo kuendelea kuwa chama
cha kishujaa katika kuwakomboa watu wake.
Pia
kuna suala zima la uwepo wa ilani ya uchaguzi ambayo ni mkataba baina ya
chama na wananchi au viongozi na wananchi ambao ndio wapiga kura
wenyewe kupitia ilani, CCM inatoa ahadi zake mbalimbali za kutekelezwa
katika muda uliopangwa wa miaka mitano.
Ni
wazi kwamba ahadi hizo zimekuwa zikitekelezwa kwa kiwango kikubwa na cha
kuridhisha kiasi cha kufanya Watanzania waendelee kuwa na imani nayo
kila uchaguzi unapowadia. Hii inajidhihirisha wazi katika chaguzi kuu
mbalimbali zilizofanyika mara tatu 1995, 2000, 2005, 2010 na 2015 ambapo
CCM iliibuka na ushindi wa kishindo
Nguzo
nyingine kuu ya CCM ni viongozi wake. Ndani ya CCM wenye dhamana ya
chama ni wanachama wenyewe na wala si viongozi. Hali hii imesaidia
kutokuwa na hata chembe au harufu ya umini wa mtu kujiona kuwa ana haki
miliki ndani ya chama au ni kiongozi wa maisha. Ikumbukwe kuwa CCM ina
haki zote kwa kiongozi yeyote yule aliyetokana na CCM.
Hiyo
ni ishara kwamba ni chama chenye misingi imara ya uongozi na ndio maana
kumekuwa na mabadiliko ya mara kwa mara ya uongozi kwa kufuata misingi
ya katiba ya chama. Kila baada ya mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi
wa mashina hadi Taifa na katika uchaguzi huo ndipo watu huingia na
kutoka.
Aidha
hali hii ni tofauti na vyama vingine nchini ambavyo walivyoviasisi ni
viongozi wa kudumu hadi hii leo. Wanapoambia kuna uchaguzi baadhi ya
viongozi hao kufanya mizengwe kwa wale wanaonyesha nia ya kuleta
mabadiliko na hata kuwafukuza.
Kwa
sasa CCM ipo chini ya Uenyekiti wa Rais Dk. John Pombe Magufuli ambaye
amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inaendelea kuongoza kupitia ridhaa
ya Wananchi.
Ridhaa
hii inatokana na CCM kuendelea kuwa na uongozi imara, sera safi,
maendeleo bora na hivyo kuendelea kuwa tegemeo la kila Mtanzania
anayependa haki na maendeleo pamoja na ustawi uliopo.
Hakuna
binadamu aliyemkamilifu kwa kila kitu isipokuwa Mungu pekee. Kwa
kulitambua hilo CCM iliona si vizuri endapo wataendelea kuwa peke yao.
Mwaka 1990 uliletwa mswada na mwaka 1992 walio wachache (20%) wakapatiwa
ushindi wa uletaji wa mfumo mpya ule wa vyama vingi.
Hivyo
CCM ndiyo mkunga na mwanzilishi wa mfumo wa vyama vingi nchini. Tangu
kuasisiwa kwake CCM imeendelea kuwa mkunga na kinara ndani ya utiriri wa
vyama mbalimbali takribani 20 vya kisiasa vya hapa nchini.
Pia
CCM hii imeendelea kuwa chama cha kimaskini kinachowakumbatia watu
maskini na hii inajidhihirisha zaidi kupitia shughuli za kimaendeleo
zinazofanywa na serikali za CCM zinazokuwa madarakani ambazo zote zina
walenga watu maskini na watu wote kwa kuwa ujumla bila ya kujali rangi,
dini wala kabila la mtu.
Lengo
la kuanzishwa kwa CCM kulikuwa na malengo ya kumkomboa Mtanzania haswa
Mkulima na mfanyakazi (kupitia nembo ya jembe na nyundo) ili kumfanya
aweze kupiga hatua kimaendeleo. Hivyo hatutakosea endapo tutasema kuwa
CCM ni chama cha kimapinduzi ya kweli na dhihiri mathalani CCM imekuwa
daima chama tawala kinachopinga maradhi, ujinga na umasikini. Vile vile
CCM kimeendelea kuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo ya kiuchumi
kijamii na kiutamaduni.
Mathalani
katika elimu, kupitia mipango yake MMEM (Mpango wa Maendeleo ya Elimu
ya Msingi) na MMES (Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari)
kumuwezesha kuwepo kea ongezeko la idadi ya Wanafunzi katika shule.
Hii
inatokana na uwepo wa sera safi ya kuhakikisha kuwa kuna shule za Msingi
katika kila kijiji na uwepo wa shule za Sekondari katika kila kata.
Hali hii imesaidia uwepo wa shule 15,816 shule za msingi na shule 2,171
kwa shule za sekondari.
Pia
Serikali za CCM zimechakalikia uwepo wa vyuo mbalimbali ambapo mpaka
sasa kuna jumla ya vyuo 47 hapa nchini toka vyuo 3 vilivyikuwepo wakati
tunapata uhuru. Mfano ya vyuo hivyo ni chuo kikuu cha Dar es salaam
“Mlimani” (UDSM) na matawi yake ambayo ni chuo cha Elimu Chang’ombe
(DUCE) ;Chuo cha Madaktari Muhimbili; Chuo cha MKWAWA; Chuo cha ardhi
(U-class).
Vyuo
vingine vikuu ni pamoja na chuo cha kilimo cha Sokoine; Chuo kikuu cha
Mzumbe, na chuo kikuu cha Dodoma (U – Dom) ambacho ni chuo kipya chenye
uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 40,000.
Upatikanaji wa maji vijijini 1961 ulikua 6% sasa ni 68%. Upatikanaji wa maji mijini 1961 ulikua 25% sasa ni 83%.
Upande wa huduma za kiafya; hospitali 1961 zilikua 48 sasa zipo 109. Zahanati 1961 zilikua 239 sasa zipo 6114.
Upande
wa Elimu; Shule za msingi 1961 zilikua 3000 sasa zipo 16538. Walimu wa
shule za msingi 1961 walikua 9885 sasa wapo 88905. Shule za sekondari
1961 zilikua 41 sasa zipo 4753. Walimu wa sekondari mwaka 1961 walikua
764 sasa wapo 88908.
Kwa
mujibu wa Baraza la Mitihani NECTA ni kwamba mwaka 2016 ufaulu wa jumla
umeongezeka kwa asilimia 2.56 kutoka asilimiq 67.53 mwaka 2015 hadi
asilimia 70.09 mwaka 2016.
Upande
wa Miundo mbinu, tulikua na km za barabara za lami 1300 zenye ukubwa wa
kilomita 33,600 mwaka 1961 na sasa kuna kilomita 124,234 na zingine
zinaendelea kukamilika kujengwa.
Serikali
za CCM zimefanikiwa kuleta unafuu katika elimu na hata kuleta unafuu wa
wanafunzi na kwa wazazi ama walezi wao kwa kuhakikisha kuwa elimu ya
shule ya msingi ni lazima kila mtoto wa miaka saba na inatolewa bure;
kila Mtanzania awe na elimu angalau ya kidato cha nne; kuondoa kero za
ada za mitihani kwa shule za msingi na sekondari.
Wakati
tunapata uhuru (1961) kulikuwa na Watanzania milioni 9 kati ya hao ni
watu wasiozidi laki tatu waliobahatika kupata elimu ya darasani na
waliokuwa darasani kipindi hicho hawakufika wanafunzi 1,500.
Takribani
miaka 56 sasa baada ya uhuru, CCM imeendelea kuliongoza taifa letu
lenye watu wapatao Milioni 45 (kwa mujibu wa sensa ya watu iliyofanyika
nchini mnamo mwaka 2012) kwa kuhakikisha wanapatia elimu ya kutosha na
yenye viwango. Leo hii asilimia kubwa ya Watanzania wameelimika hadi
elimu ya ngazi ya chuo, na kwa mujibu wa takwimu za sasa kuna wanafunzi
wapatao milioni 15 wakiendelea na masomo yao kwa ngazi mbalimbali kati
ya hao kuna wanazuoni wapatao 120,000.
Hata
kwa upande wa mikopo ya elimu ya juu nako CCM ipo bega kwa bega na jamii
kwa kuhakikisha kuwa kila Mwanachuo anapatiwa mkopo wa gharama za elimu
ya juu kwa kadri uwezo wa kifedha utakavyokuwa.
Katika mwaka wa masomo
wa 2005/2006 Bodi ya Mikopo ilitoa mikopo kwa wanafunzi 42,729
iliyogharimu sh. bilioni 56.1 na mwaka wa masomo wa 2016/2017 bodi ya
mikopo ilitoa mikopo iliyogharimu shilingi bilioni 487 kwa hapa nchini
kuna changamoto kubwa cha kiwango hiki lakini tusisahau ya kwamba
kiwango hiki na idadi hii ya wanafunzi wanaonufaika ni kikubwa mno
ambacho hakiwezi kufikiwa na nchi yeyote ile ya Afrika Mashariki na
kati. Nani kama CCM?
Hata
kwenye mapambano ya dhidi ya ‘maradhi’ nako jitihada si za kubezwa.
Tumeshuhudia ujenzi wa vituo vya afya kwenye kila kijiji na ujenzi wa
zahanati kwenye kila kata Kwa mfano jumla ya Zahanati 5,422 na vituo vya
afya 663 vimejengwa ndani ya utawala wa CCM. ; pia kuna uwepo wa
hospitali kubwa kila mkoa mathalani Muhimbili hapa Dar es salaam,
Bugando kule Mwanza na kadhalika.
Serikali
za CCM hazina mzaha katika mapambano ya dhahiri dhidi ya Malaria, kifua
kikuu, ukoma, matende trakoma, saratani za aina zote. Pia kuna
mapambano dhidi ya magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu,
kichocho, homa ya mafua ya ndege na yale mafua ya nguruwe.
Licha
ya hapo, pia kumekuwa na maboresho ya dhati ya Afya ya mama na mtoto,
upungufu wa vifo vya uzazi kwa utoaji wa elimu ya uzazi, kuongeza idadi
ya wakunga na utoaji wa huduma ya kujifungua katika kiwango cha hali ya
juu.
Katika
kuhakikisha kuwa kila mtu maskini na asiyejiweza anapatiwa huduma sawa
na sahihi kumekuwa na sera safi ya utoaji wa huduma bure za matibabu kwa
makundi maalum kama vile walemavu ,vipofu, wazee wa zaidi ya miaka 60,
na watu maskini wasiojiweza ilimradi tu apatiwe uthibitisho kutoka kwa
Serikali za mitaa.
Pia
kuna utoaji bure wa huduma za matibabu kwa magonjwa ya milipuko ndani ya
jamii na hata pia wale wahanga wa majanga mbalimbali hawajasahaulika.
Jamani kama haya si mafanikio ya Serikali za CCM ni kitu gani hasa?
Wahenga
walisema, ‘Mnyonge mnyongeni, lakini haki zake mpeni’.
Licha ya maneno
mengi mno yasiyo na tija kusemwa semwa mitaani lakini kwa upande wa
Serikali za CCM hawajavunjika moyo na daima wanazidi kusonga mbele kwa
mbele. Baadhi ya viongozi kulumbana, ama matokeo ya uchaguzi kuteteleka
ni sehemu tu mapito ya chama chochote kile cha kisiasa hapa Duniani
ambapo unachukuliwa kama msingi mkuu wa maboresho ya chama husika.
Sote
kwa pamoja tumeshuhudia na ujenzi na maboresho ya miundombinu, hakikisho
la kilimo safi, mapambano dhidi ya ubadhilifu wa mali za umma,
mapambano makali ya rushwa na ufisadi nchini, uanzilishwaji wa vyanzo
vya ndani ya mapato ili tuweze kujitegemea wenyewe na kadhalika.
Tawala
zote za CCM zilielewa ile dhana ya kuwa nchi haiwezi kuwa na mazingira
mazuri ya kiuchumi iwapo miundombinu ya uchukuzi na usafirishaji itakuwa
duni na isiyotosheleza mahitaji.
Katika
serikali zake zimeendelea na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya
nchi bila ya kujalisha ni nani anaongoza na ni kwa awamu gani. Hata
katika utawala wa awamu ya tano ya Rais Magufuli ameendeleza kazi nzuri
na safi iliyofanywa na waliomtangulia.
Serikali
za CCM hazina mzaha kabisa katika kuhakikisha kuwa rasilimali
tulizonazo zinawasaidia Watanzania na kuhakikisha wanakusanya kodi
ipasavyo kwa kukuimarisha vyanzo vilivyopo pamoja na kuanzisha vyanzo
vipya ambapo mpaka mwaka huu 2017 mapato ya nchi yetu yameongezeka mara
dufu hadi kufikia shilingi Trilioni 1.5 kwa mwezi mmoja. Nani kama CCM?
Serikali
za CCM zimeendelea kufanya mengi mazuri ambapo kwa upande wa Zanzibar
imefanikiwa kuondoa viashirio vya mvunjiko wa mshikamano, amani na
utulivu waliokuwa nao kwa kuiondoa ile hali iliyotaka kuwatawala ya
kununiana, kutokusalimiana, hadi ilifika kipindi watu walishindwa
kuzikana.
Leo hii hali ni tofauti kabisa kwani ile hali ya aibu
imeshawaondoka na ule umoja wa Kitaifa, upendo, mshikamano na nguvu ya
pamoja imerejea tena. Yote hayo yamewezekana chini ya himaya za utawala
wa CCM.
Nyakati
zote chama cha mapinduzi wameonekana kuguswa na kero na shida za
Watanzania kwa kukata kiu ya kwikwi ya umaskini wa watu wake kwa
kuwaletea maendeleo ya kweli. Hakika CCM ndio mama na mama ndio ajuaye
uchungu wa mwana.
Mathalani
kwa upande wa kilimo. Serikali za CCM haziko nyuma kwenye harakati za
mapigano ya kilimo bora hapa nchini. Imefahamika kwamba zaidi ya
asilimia 80 ya Watanzania ni wakulima ambao wanategemea kilimo kama
nguzo ya maisha yao. Katika kuhakikisha kuwa kilimo kinaboreka zaidi na
kuepusha mabalaa ya njaa kumekuwepo na uanzishaji wa kauli mbiu
mbalimbali za kilimo.
Kauli
mbiu hizo za kilimo ni kama vile, kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa
(1967); Siasa ni kilimo (1971); Kilimo cha kufa na kupona (1974); na
kilimo kwanza (2009). Hakika matokeo chanya ya harakati za sera hizo
zimekuwa zikionekana kwa dhahiri.
Katika
idara ya ubadhilifu wa mali za umma nako harakati za mapambano hazikuwa
nyuma. Tumeshuhudia idara mbalimbali zikibanwa mbavu kwa uthibiti imara
kabisa tofauti na mitazamo hasi ya baadhi ya watu yalivyo. Mifano
husika ni katika idara za maliasili, uvuvi, bandari, madini, chakula
ambapo kote kumekuwa na uthibiti tulioshuhudia wa mapato na rasilimali
za Watanzania.
CCM
hii hii imekuwa mstari wa mbele kupambana na mafisadi (hawa ni wahujumu
uchumi wanaotafuna rasilimali na mali za umma) Serikali za CCM imeweza
kuvipa nguvu idara za kisheria ili kuweza kupambana na aina yeyote ilaya
ubadhilifu na uhujumu uchumi. Kwa kutambua mgawanyo wa mihimili ya
madaraka vimeachiliwa vyombo husika kufuatilia ili haki ipatikane bila
kuhujumu upande wowote. Huu ndio utawala wa kisheria.
Mbali
na hayo yapo mambo mengi ambayo CCM imefanya mapinduzi zaidi kupitia
sera na ilani ambazo zipo kwa ajili ya kumlinda, kumtetea na kumkomboa
mtu wa tabaka la chini na kati ambao ndio , asilimia kubwa ya
Watanzania.
CCM
inaundwa na Wanadamu ambapo inafahamika vyema kuwa Binadamu si Malaika
hajakamilika na kwa kuwa CCM ipo kama Mwanadamu nayo pia haijakamilika,
kuna sehemu imefanya vizuri sana, kuna sehemu imefanya vizuri na kuna
sehemu pia haijafanya vizuri. CCM kama chama cha kisiasa chchote kile
Duniani hakitaweza kumridhisha kila Mtu kwa kiwango kile kinachotaka.
Lakini
hali hiyo haitaweza kufuta mazuri ambayo CCM kupitia serikali zake
zilizokuwa na iliyopo madarakani kujivunia mafanikio yaliyopatikana toka
enzi za kulikomboa Taifa letu toka kwa wakoloni Waingereza mpaka hapa
ilipoifikisha.
Wakati
CCM ikiadhimisha miaka 40 ya kumbukizi ya kuzaliwa kwake haina budi
kubadilika na kuendana na kasi ya Mwenyekiti wake Rais Magufuli,
kuendana na kasi ya Hapa Kazi Tu. Heri ya kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi.
Na Emmanuel J. Shilatu
0767488622

No comments