Chama cha Wakandarasi Tanzania waomba kupewa nafasi kuijenga Dodoma, wampongeza Rais Magufuli
Wakizungumza mapema leo 17 Februari 2017, Jijini Dar es Salaam, uongozi wa chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, wamebainisha kuwa wanafikisha ombi lao kwa Mheshimiwa Rais kuhusiana na tamko la hivi karibuni lililotolewa na Serikali kwa Wakala wa Majengo nchini (TBA) na baadhi ya taasisi za Umma hapa nchini, kukabidhiwa uhimili wa kushughulikia ujenzi wa miradi ya umma hasa majengo.
“Kwa vyovyote vile tunatarajia msukumo mkubwa katika kutekeleza azma hiyo. Na hivyo basi matarajio ni wakandarasi wa hapa nchini kushirikishwa katika zabuni mbalimbali za miradi ya Umma.
Hivyo basi, ombi letu kwa Serikali ya awamu hii ya tano, ni kuwashirikisha katika zabuni zake wakandarasi woet wa Kitanzania, wakiwemo Wakandarasi wa madaraja yote ili waweze kujijenga kitaalam katika utekelezaji miradi na kuongeza ajira ya vijana katika makampuni hayo” ameeleza Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, Injinia Lawrence Mwakyambiki wakati wa mkutano huo kwa waandishi wa habari.
Aidha, Mwenyekiti huyo Taifa, amesisitiza kuwa, ombi la chama chao kwa Rais Magufuli linazingatia maazimio yaliyopitishwa katika mikutano ya majadiliano kati ya Bodi ya Wakandarasi Tanzania na Wakanadarasi wenyewe iliyofanyika Mei 2016 ambapo waliazimia taasisi za Umma pamoja na Wizara kuwa na miradi ya kipekee wa lengo la kujenga uwezo wa Wakandarasi wa Kitanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakandarasi Tanzania kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia John Bura amebainisha kuwa, Wakandarasi wa Tanzania wamekuwa katika mstari wa mbele katika kufanya kazi za kizalendo hivyo wanapongeza juhudi za Rais Magufuli kwa kuwajali wakandarasi wa ndani.
“Tunashukru Rais Magufuli na wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS kwa kuitikia wito wa Wakandarasi kutengewa miradi michache ambayo ilikwisha tangazwa, Tunapongeza sana kwa hilo na salamu zetu zifike kwa Rais wetu” ameeleza Injia Bura.
Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania (CATA) pia kimewaomba wanachama wake kote nchini kujitokeza na kulipia malipo yao ya ada yaliyo kisheria ili kufanikisha malengo ya chama hicho.
Mwenyekiti
Taifa wa Chama hicho cha Wakandarasi Tanzania, Injinia Lawrence
Mwakyambiki (kulia) akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani)
wakati wa mkutano huo waandishi wa habari.
Mwenyekiti
wa Wakandarasi Tanzania kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia John Bura
akizungumza na waandishi wa Habari (Hawapo pichani)
No comments