Meya Mwita afichua siri ya wanafunzi DSM kufeli
Mwita ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam katika sherehe za Maulidi ya Kumswalia Mtume Mohamed (S.A.W) iliyoandaliwa na Mjumbe wa Kamati ya Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Kinondoni, Sheikh Daruwesh Dume.
“Watoto wetu wamekua wanapata matokeo mabaya ya mtihani, moja ya sababu za watoto kufeli ni baadhi ya wazazi au walezi wao kuwapa pesa nyingi ambazo hutumia kufanya anasa ikiwemo kununua simu za kisasa smart phone, ambazo hutumia katika mitandao ya kijamii,” amesema na kuongeza.
“Mtoto wa kidato cha kwanza unamnunulia smart phone, huu si mtihani? Badala ya kusoma wanaishia kutumia mitandao ya kijamii. Niwaombe wazazi muwanyime watoto pesa za anasa bali muwafundishe mafundisho ya dini ili wawe watoto wema wenye kuzingatia masomo yao.”
Aidha, Mwita ametoa wito kwa wazazi na walezi kushirikiana na serikali kutatua changamoto zilizo katika sekta ya elimu ambazo ziko chini ya uwezo wao ikiwemo pesa na vifaa vya ujenzi wa madarasa.
“Watoto wanasoma kwa tabu utakuta darasa moja wanakaa watoto zaidi zaidi ya mia. Najua wapo wazazi na walezi wenye vipato vizuri, kwa nini msichangie hata ujenzi wa madarasa? Hata kama elimu inatolewa bure lakini bado kuna changamoto zinazosababisha kiwango cha ufaulu kushuka ikiwemo uhaba wa madarasa,” amesema.
No comments