MAHAKAMA YAMFUATA MANJI HOSPITALI, ASOMOMEWA MASHTAKA YA UHUJUMU UCHUMI
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu leo imelazimika kuhamishia shughuli zake katika
Hospitali ya taifa ya Muhimbili kwa muda kumsomea mfanyabiashara
Yusufali Manji (41), mashitaka ya uhujumu uchumi yanayomkabili.
Manji
amesomewa mashtaka hayo katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete
iliyopo Hospitalini hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mhe. Huduma Shaidi.
Katika
kesi hiyo, Manji anashitakiwa pamoja na wenzake watatu, Meneja
Rasilimali watu wa Kampuni ya Quality Group Ltd, Deogratius Kisinda
(28), Mtunza stoo, Abdallah Sangey (46) na Thobias Fwere (43) mkazi wa
Chanika, ambapo wote watatu wamesomewa mashtaka yao katika Mahakama hiyo
kabla haijahamia hospitali ya Muhimbili kuanzia muda wa saa Tisa
alasiri na kumalizika saa 16:41 (saa kumi na dakika arobaini na moja).
Mahakama
ilifikia uamuzi wa kuhamia Muhimbili baada ya Manji kuwa amelazwa
Hospitalini hapo akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kulazimika kusomewa
mashtaka yake akiwa kitandani.
Akisoma
mashtaka hayo, wakili Mwandamizi wa Serikali, Tulumanywa Majigo amedai,
Juni 30, mwaka huu huko Chang’ombe A wilayani Temeke jijini Dar es
Salaam, washitakiwa wote kwa pamoja, walikutwa na askari polisi wakiwa
na mabalo 35 ya vitambaa vinavyotumika kutengenezea sare za Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vyenye thamani ya milioni 192.5.
Imedaiwa
kuwa, Julai Mosi mwaka huu, maeneo hayo hayo, washitakiwa wote
walikutwa na askari polisi wakiwa na mabalo nane ya vitambaa
vinavyotumika kutengenezea sare za JWTZ vyenye thamani ya milioni 44.
Aidha
imedaiwa kuwa, Juni 30, washitakiwa hao walikutwa wakiwa na mhuri wa
JWTZ ambao uliandikwa ‘’Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha JWTZ’’ bila kuwa
na uhalali kitendo kinachohatarisha usalama wa nchi.
Washtakiwa
pia Pia wanadaiwa, kukutwa na mhuri uliokuwa umeandikwa ‘’Kamanda
Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma bila kuwa na uhalali kitendo
kinachohatarisha usalama.
Majigo
aliendelea kudai kuwa mnamo Juni 30, mwaka huu maeneo hayo hayo,
washitakiwa kwa pamoja walikutwa na mhuri ulioandikwa ‘’Commanding
Officer 835 KJ, Mgambo P.o.Box 224 Korogwe isivyo halali.
Manji na mwenzake wamedaiwa kukutwa na gari lenye namba za usajili SU 383 mali waliyojipatia isivyo halali. Gari jingine wanalodaiwa kukutwa nalo washitakiwa ni lenye namba za usajili SM 8573 pasipo uhalali.
Washitakiwa
hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa sheria ya uhujumu uchumi na ya
usalama wa Taifa haijaipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi hiyo.
Mawakili
wa Serikali wakiongozwa na Mawakili waandamizi Mutalemwa Kishenyi,
Nassoro Katuga na Majigo, walisema upelelezi wa shauri hilo
haujakamilika na kwamba wamepata hati ya kupinga dhamana kutoka kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP).
Wakili
Katuga alidai kuwa DPP anaomba ruhusa washitakiwa wasiruhusiwe kupewa
dhamana kwa sababu wakiachiwa watahatarisha usalama na maslahi ya nchi. Pia alidai kwenye mashitaka ya kwanza na ya pili, mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kushughulikia masuala ya dhamana.
Hata
hivyo, Wakili wa utetezi, Hudson Ndusyepo, alipinga hoja zilizotolewa
na upande wa mashitaka kwamba mashitaka hayo yanaiondolea mahakama
kufikiria suala la dhamana kwa washitakiwa.
Ndusyepo
alidai upande wa mashitaka umekuwa na nia mbaya ya kuwasilisha hati ili
kupinga dhamana na kudai kuwa kitendo hicho ni matumizi mabaya ya
madaraka ambayo hawawatendei haki washitakiwa.
Hata
hivyo, Hakimu Shaidi alisema kuwa masuala hayo yalitakiwa kuongelewa
katika mahakama yenye mamlaka ambayo ni Mahakama Kuu na kwa sababu DPP
hajaipa mamlaka mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo, hivyo hawezi
kuzungumza chochote.
Kesi
hiyo imeahirishwa hadi Julai 19, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na
washitakiwa watatu wamerudishwa rumande huku mshitakiwa Manji, amebaki
chini ya uangalizi wa polisi na baadaye Magereza kwa kipindi chote
atakachokuwa hospitalini hapo, na kuhamishiwa mahabusu baada ya kupata
nafuu.
No comments