Waziri Mkuu amtumbua DED wa mbozi kwa matumizi mabaya ya fedha za umma
Katika
kuhakikisha kunakuwepo na matumizi mazuri ya fedha za umma, Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri
ya wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe, Eliseyi Mgoyi pamoja na maofisa
wengine watatu kwa tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma.
Majaliwa
amewasimamisha kazi maofisa hao mapema hii leo wakati alipozungumza na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwenye ukumbi wa Shule ya
Sekondari Vwawa, akiwa katika ziara yake ya kikazi.
Amesema
kuwa Maofisa hao wamekiuka sheria za matengenezo ya magari ya Serikali
kwa kwenda kutengeneza katika gereji ambazo hazikusajiliwa na wala
hazifanyi shughuli hiyo, jambo ambalo halikubaliki.
“Halmashauri
inanuka rushwa tunataka iwe safi. Hatuwezi kukubali kuona Halmashauri
hii na zingine nchini zikigeuzwa kuwa magenge. Kwa Serikali hii no,
hatuhitaji rushwa wala harufu ya ufisadi.”amesema Majaliwa
Aidha,
amesema kuwa Serikali haiwezi kuvumilia kuona watumishi waliopewa
dhamana wakijinufaisha kwa fedha za umma na kuwaacha wananchi
wakiendelea kuteseka kwa kukosa huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za
maji, afya na elimu, hivyo itaendelea kuwachukulia hatua.
Hata
hivyo, Majaliwa amewataka Madiwani na Wakuu wa Idara katika Halmashauri
zote nchini wabadilike na wahakikisha wanashirikiana na kufanya kazi
kwa ushirikiano kwani wakigawanyika watashindwa kutekeleza majukumu yao
ya kuwatumikia wananchi.

No comments