NHC yaagizwa kujenga nyuma katika maeneo yote mapya ya utawala
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameliagiza Shirika la nyumba Nchini kwenda kujenga
nyumba bora za makazi katika maeneo yote mapya ya utawala ikiwemo mikoa
na wilaya ili kusaidia kutatua changamoto ya makazi kwa watumishi.
Pia
ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 20 za watumishi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe zinazojengwa katika
kijiji cha Tindingoma, unaojengwa na Shirika la Nyumba Nchini.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana (Ijumaa, Julai 21, 2017) wakati
akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye
kijiji cha Naming’ongo wilaya ya Momba akiwa katika ziara yake ya kikazi
mkoani Songwe.
“Nalipongeza
Shirika la Nyumba kwa mikakati waliyonayo ndani ya shirika hilo na
kwamba waendelee na utekelezaji wa mipango hiyo ya ujenzi wa nyumba ili
maeneo yote mapya ya utawala yaweze kuwa na makazi bora ya kuishi
watumishi.”
Pia
aliwataka wakazi wa kata ya Chitete yaliko makao makuu ya wilaya ya
Momba kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa makao makuu wa wilaya
kwenye kata yao kwa kujenga nyumba za kisasa kwa ajili ya kupangisha
watumishi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Nehemia Mchechu amesema mradi
huo wenye thamani ya sh bilioni 2.2 ulianza kujengwa Machi 2016 na
unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Amesema
mradi huo ulibuniwa baada kupokea maombi kutoka Halmashauri ya wilaya
ya Momba na kwamba unatekelezwa kwa awamu mbili ya kwanza ni ujenzi
nyumba nane na tayari zimekamilika.
Ameongeza
kwamba ujenzi wa awamu ya pili unajumuisha nyumba tisa ambapo gharama
ya ujenzi wa nyumba itatumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya
ofisi za Halmashauri hiyo.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya NHC , Bi. Blandina Nyoni amesema shirika hilo
lilianzisha mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu katika maeneo
mbalimbali nchini ili kuwawezesha wananchi kuwa na makazi bora.
Amesema
katika miradi 54 ya ujenzi wa nyumba inayotekelezwa na shirika hilo
katika maeneo mbalimbali nchini kati yake miradi 24 imekamilika ikiwemo
14 ya nyumba za gharama nafuu.
Pia
Mbunge wa jimbo la Momba (CHADEMA), David Silinde amesema anashukuru
Serikali kwa ujenzi wa nyumba hizo na kumueleza Waziri Mkuu kwamba
wananchi wa Momba wanaridhishwa na utendaji wa Serikali na kwamba
maendeleo hayana chama.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, JULAI 21, 2017

No comments