RPC ARUSHA : TUMEPUNGUZA UHALIFU KWA 24%
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupunguza makosa ya
jinai kwa mwaka huu 2017 toka 1,378 yaliyoripotiwa mwaka jana 2016 hadi kufikia
1,041 na kufanya idadi ya makosa yaliyopungua
kufikia 337.
Akitoa takwimu hizo ofisini kwake jana mchana, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha
Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo, alisema kwamba punguzo hilo ni sawa na
asilimia 24.4 huku akifafanua kwamba takwimu hizo ni kwa mujibu wa kuanzia mwezi
Januari hadi Juni mwaka huu 2017.
“Huu upungufu wa makosa ya jinai ni takwimu za nusu mwaka,
toka Januari hadi Juni mwaka huu 2017 ikilinganishwa na mwaka 2016 kwa muda
kama huo, hivyo utaona tumejitahidi “. Alifafanua Kamanda Mkumbo, huku
akiendelea kubainisha,
“Mwaka jana kwa nusu mwaka makosa ya mauaji yalikuwa 45
lakini mwaka huu kwa kipindi kama hicho makosa yalikuwa 36 pungufu ya makosa 9,
wakati makosa ya kubaka yalikuwa 106 kwa mwaka jana lakini mwaka huu yameshuka
hadi kufikia makosa 79 pungufu ya makosa 27, huku makosa ya unyang’anyi wa
kutumia silaha mwaka jana yalikuwa makosa 16 na mwaka huu kwa kipindi kama
hicho yamekuwa makosa matatu sawa na upungufu wa makosa 13”. Alisema Kamanda
Mkumbo.
Akiendelea kutoa takwimu hizo Kamanda Mkumbo aliendelea
kusema kwamba, makosa ya unyang’anyi wa kutumia nguvu kwa miezi sita ya mwanzo wa
mwaka jana yalikuwa 54 na mwaka huu kwa kipindi kama hicho yalifikia makosa 28
ni pungufu ya makosa 26, makosa ya wizi wa pikipiki kwa mwaka jana yalikuwa 54
lakini mwaka huu yamefikia 24 pungufu ya makosa 30 na makosa ya uvunjaji
yalikuwa 453 kwa miezi sita ya mwaka jana lakini mwaka huu yameshuka hadi
kufikia 195 pungufu ya makosa 258.
Akizungumzia mapambano dhidi ya dawa za kulevya Kamanda
Mkumbo alisema kwamba ongezeko la ukamataji lilipanda toka kesi 295 hadi
kufikia kesi 301 huku akielezea hilo linatokana na zao la ushirikiano wa
wananchi na Jeshi la Polisi ambapo taarifa wanazozitoa zinafanyiwa kazi hasa
kupitia misako inayofanyika katika maeneo mbalimbali.
Aidha kwa upande wa usalama barabarani Kamanda Mkumbo alisema
jeshi hilo kwa miezi sita ya mwaka huu yaani Januari hadi Juni lilikusanya
jumla ya Tsh 2,107,530,000/= (Bilioni mbili milioni mia moja na saba laki tano
na elfu thelathini) kutokana na tozo za makosa ya usalama barabarani kiasi
hicho ni tofauti na mwaka jana 2016 kwa miezi sita ya mwanzo ambapo tozo
zilizokusanywa zilikuwa Tsh 2,520,180,000/= (Bilioni mbili milioni mia tano
ishirini laki moja na elfu themanini).
Hii ni pungufu ya tozo zenye thamani ya Tsh 412,650,000/=
(Milioni mia nne kumi na mbili laki sita na elfu hamsini) kwa mwaka huu na hali
hiyo ilitokana na elimu iliyotolewa na Jeshi hilo kupitia kikosi cha usalama
barabarani kwa makundi mbalimbali ya watumiaji wote wa barabara wa vyombo vya
usafiri hasa waendesha pikipiki maarufu kama boda boda na watembea kwa miguu.
Mafanikio hayo ni sehemu ya
muendelezo wa mapambano dhidi ya uhalifu ambapo takwimu za uhalifu kwa
mwaka nzima wa 2016 zinaonyesha makosa ya jinai yalipungua kwa asilimia
6.8 ikilinganishwa na mwaka juzi 2015.
No comments