WAMILIKI WA MABASI YA ABIRIA WAPEWA ONYO
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limetoa onyo kwa wamiliki wa
mabasi ambayo yanavunja sheria za usalama barabarani. Akizungumza na waandishi wa habari leo mchana ofisini
kwake wakati akitoa taarifa ya matokeo ya ukaguzi wa mabasi ya abiria
uliofanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia tarehe 22 mwezi huu hadi 24,
Kamamda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema kwamba, wamiliki wa magari wanatakiwa
wahakikishe mabasi yao yanazingatia ubora unaokubalika hali ambayo itasaidia abiria
wanasafiri salama.
“Mbali na ubora wa gari lakini pia madereva wanatakiwa
wazingatie sheria za usalama barabarani kama vile kuendesha kwa kufuata
maelekezo ya alama“. Alisema Kamanda Mkumbo.
Alisema katika ukaguzi huo wa kushtukiza uliojumuisha mabasi
yaliyokuwa yanakwenda mikoani na yale yaliyokuwa yanaingia jijini hapa, jumla
ya mabasi 77 yalikamatwa kwa makosa ya
ubovu na mwendokasi.
“Kati ya hayo mabasi 25 yalikamatwa kwa makosa ya mwendokasi
ambapo 20 kati yao yalilipiwa tozo na matano wahusika walipelekwa mahakamani,
wakati mabasi 52 yalikutwa na makosa ya ubovu ambapo 41 yalitozwa tozo na mabasi
11 toka makampuni mbalimbali tumeyasitishia kutoa huduma mpaka hapo yatakapofanyiwa
marekebisho”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Kamanda Mkumbo alisema kwamba pamoja na ukaguzi wa magari
hayo ambao unafanywa kila siku lakini Jeshi hilo litaendelea kufanya kaguzi za
kushtukiza mara kwa mara ili kuhakikisha abiria wa mabasi hayo wanasafiri
salama, huku akitoa wito kwa abiria watoe taarifa popote wanapogundua dereva
anakwenda kinyume na sheria za usalama barabarani.
No comments