PROF. MBARAWA AWATAKA TBA KUMALIZA NYUMBA YA JAJI MFAWIDHI
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto),
akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Tellack, mara baada
ya kuwasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto),
akifafanua jambo kwa viongozi wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara
alipokutana nao mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Meneja
wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Shinyanga Eng. Amosi
Manyete akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa
Makame Mbarawa, mfumo wa maji taka uliowekwa nje ya jengo la Mahakama
Kuu ya Tanzania, kanda ya Shinyanga iliyopo mkoani humo. Kushoto ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda hiyo Mhe. Jaji Richard Kibella.
Muonekano
wa jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga ambalo
limekamilika na ujenzi wake umesimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA).
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua
moja ya nyumba za watumishi eneo la Rubaga zinazojengwa na Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), mkoani Shinyanga.
Muonekano wa jengo la Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambalo ujenzi wake unasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameutaka
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kuhakikisha ndani ya miezi sita
wanakamilisha ujenzi wa nyumba ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya
Shinyanga.
Prof.
Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani humo wakati alipokagua miradi
mbalimbali inayotekelezwa na Wakala huo ambapo pamoja na mambo mengine
amesisitiza umuhimu wa kuwapatia waheshimiwa majaji mahali pazuri pa
kuishi ili waweze kutimiza wajibu wao wa kutenda haki kwa wananchi
ipasavyo.
“Hakikisheni
mnakamilisha ujenzi wa nyumba hii haraka iwezekanavyo ili Mheshimiwa
huyu apate mahali pazuri pa kuishi, kufanya hivi kutarahisisha majukumu
yake na kufanikish utendaji wa kazi”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amesisitiza
umuhimu wa Wakala huo kuongeza kasi katika miradi mbalimbali
inayoendelea ya ujenzi wa nyumba za viongozi ili kuondoa adha ya kodi za
pango kubwa zinazopotea kwa viongozi hao kupanga kwa watu binafsi.
Naye,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga Mhe. Jaji Richard
Kibella amemshukuru Prof. Mbarawa kwa niaba ya taasisi zake za TBA na
Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kwa namna ambavyo wameshirikiana na
Mahakama kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na kuwapatia huduma nyingine
za uendeshaji.
Aidha,
ameiomba Serikali kukamilisha kwa haraka ujenzi wa nyumba za viongozi
na watumishi wa mahakama kwani gharama kubwa zinatumika katika malipo ya
upangaji wa nyumba za viongozi.
“Mhe.
Prof. Mbarawa suala la nyumba ni changamoto, nyumba za kupanga zina
gharama kubwa ambapo kwa namna moja au nyingine inaongeza gharama za
uendeshaji wa mahakama na kupunguza usalama”, amefafanua Jaji Kibella.
Kwa
upande wake Mtendaji wa Mahakama hiyo Bwana Ernest Masanja, amemueleza
Prof. Mbarawa kuwa kukamilka kwa jengo la Mahakama hiyo kumewezesha
Majaji na watendaji wengine wa mahakama kufanya kazi kwa bidii, ufanisi
na kwa wakati katika kuwapatia wananchi haki.
Katika
hatua nyingine, Prof. Mbarawa ametembelea na kukagua maendeleo ya mradi
wa ujenzi wa Hospitali ya Mkoa huo unaosimamiwa na TBA na ameuelekeza
Wakala huo kushirikiana na Mamlaka husika kuhakikisha kuwa ujenzi wake
unazingatia viwango na ubora na kukamilika kwa wakati.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments