HAKIMU KESI YA UCHOCHEZI YA MBUNGE LEWA AJITOA KISA 'USHOSTI'
ARUSHA
HAKIMU wa Mahakama ya Wilaya Arusha,
Patricia Kisinda amejitoa kwenye kesi namba 441/2016 ya uchochezi dhidi
ya Rais John Magufuli inayowakabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza jana mahakamani hapo, Hakimu
Kisinda alisema amekubali ombi la Wakili wa Serikali, Sabina Silayo la
kumwomba ajitoe kutokana na urafiki na mke wa ndoa wa Lema.
“Ili kutendeka kwa haki pande zote mbili
kwenye kesi hii, nakubaliana na ombi lililotolewa mahakamani hapa na
najitoa, lakini haki ya kukata rufaa ipo wazi kwa asiyeridhika na uamuzi
huu wa kujitoa,” alisema hakimu Kisinda.
Kabla ya kujitoa, Wakili Silayo aliomba
hakimu ajitoe kwa sababu upande wa Jamhuri hawana imani naye, hivyo bora
ajiondoe sababu ana uhusiano na mke wa ndoa wa mshitakiwa Lema na
ushahidi wanao na halina pingamizi, “hivyo hatutatendewa haki, itakuwa
busara hakimu akijiondoa”.
Akijibu ombi hilo, Wakili wa mshitakiwa,
Sheck Mfinanga alisema Lema anaumwa na alikuwa anarejea Arusha akitokea
bungeni Dodoma na alipofika Dar es Salaam alijisikia vibaya na
kuwasilisha nakala ya hati ya matibabu, huku akidai nakala halisi
atawasilisha.
Pia alipinga Hakimu Kisinda kujitoa kwa
madai kuwa Watanzania wote ni marafiki na ndugu na sababu lazima ipimwe
uzito na waangalie sababu za hakimu kujitoa, hivyo hoja hizo hazina
mashiko.
“Ningefurahi niletewe ushahidi wa
urafiki wa mke wa Lema na hakimu huyu, ili tuone kama kuna ukweli, maana
hoja hii haina mashiko,” alidai Mfinanga. Hata hivyo, Hakimu Kisinda
alipanga kesi hiyo Agosti 2, mwaka huu.
No comments