Rais Magufuli Azuia Hati ya kusafiria ya Mkandarasi
Akiendelea na ziara yake mkoani Lindi, Rais Dkt Magufuli amekagua
miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo na kutoa maagizo ili
kuhakikisha wananchi wananufaika na jitihada za serikali za kuboresha
maisha yao.
Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi
kumnyang’anya pasi ya kusafiria (passport) Mkandarasi anayeshughulikia
Mradi wa Maji wa Ngapa hadi hapo atakapokamilisha mradi huo.
Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokwenda kukagua mradi huo wa maji
ambao hadi sasa umetumia miaka 6 kujengwa lakini bado haijakamilika.
Pamoja na kuagiza pasi ya mkandarasi ichukuliwe, Rais Magufuli amempa
miezi miwili mkandarasi huyo kuhakikisha mradi unakamili huku RC Zambi
akiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mkandarasi hatoki eneo hilo la
mradi.
Mradi huo unaotarajiwa kumaliza tatizo la maji mkoani Lindi umegharimu
TZS bilioni 29 ambapo hadi sasa mkandarasi amelipwa bilioni 21. Rais
Magufuli amesema kuwa kama tatizo ni fedha ndio sababu mradi haumaliziki
aambiwe ili atoe fedha serikali kuu kukamilisha wananchi waweze kupata
maji.
Mradi huo wa maji ukikamilika unatarajiwa kuzaliwa maji zaidi ya lita milioni 6 kwa siku.
Rais Magufuli anatarajiwa kukamilisha ziara yake mkoani Lindi leo jioni
ambapo ataanza safari ya kwenda mkoani Mtwara atapofanya ziara yake
Jumamosi na Jumapili. Katika kuhitimisha ziara yake ya siku nne katika
mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, Rais Magufuli atahutubia mkutano wa
hadhara katika uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

No comments