MBOWE ANG’ANG’ANIWA TENA MAHAKAMANI
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyodai kuwa imeshindwa kuwapata kwa kutumia hati za wito za Mahakama, Freeman Mbowe, mkewe Dk Lilian Mtei na aliyekuwa Meneja wa Klabu ya Bilicanas, Steven Mligo kujibu mashtaka yanayowakabili, jana ilisaidiwa namna ya kuwafikia watu hao.
Mahakama
ya Wilaya ya Ilala, ilitoa barua ya wito wa kuwataka wahudhurie
mahakamani Machi 21, baada ya kufikia uamuzi wa kutoa wito huo kupitia
magazeti.
Mbowe
ambaye ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na
mkewe, Dk Mtei ni wakurugenzi wa Kampuni ya Mbowe Hotels Ltd.
Wawili
hao pamoja na Mligo, Katika kesi hiyo namba 402 ya mwaka 2016,
wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kushindwa kutumia mashine za
kielektroniki (EFD) kutoa risiti kinyume na kifungu cha 86 cha Sheria ya
Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015.
Mashtaka
mengine ni kuipotosha mamlaka kwa kutoa nyaraka za uongo kinyume na
kifungu cha 84 na kushindwa kutekeleza masharti ya Sheria ya Usimamizi
wa Kodi kinyume na kifungu cha 82 cha sheria hiyo.
Wanadaiwa kutenda
makosa hayo Mei, 2016 jijini Dar es Salaam.
Imedaiwa kuwa tangu kesi hiyo ilipofunguliwa mwishoni mwa mwaka jana, imeshatajwa mara nne bila washtakiwa kufika mahakamani.
Wakili
wa TRA, Marcel Busegano aliieleza Mahakama kuwa wamejaribu kuwapelekea
washtakiwa hati za wito wa kufika mahakamani mara nne lakini wameshindwa
kuwapata.
Alidai
Meneja wa TRA Mkoa wa Ilala alijaribu kumpigia simu ya mkononi Mbowe
lakini hakumpata na, hata walipokwenda katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) anakofanya kazi mkewe, Dk Mtei pia hawakumpata.
Kutokana
na hali hiyo, TRA iliiomba Mahakama iamuru watumie tangazo gazetini
kuwaita washtakiwa mahakamani na iwapo korti itakubali ombi hilo,
tangazo litolewe kabla ya tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.
Shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ritha Tarimo litatajwa Machi 21.
Kutokanana na ombi hilo, tangazo hilo linapaswa kutangazwa gazetini kabla ya tarehe hiyo.

No comments