SERIKALI IWASHIRIKISHE WAFANYABIASHARA KUPIGA VITA RUSHWA

Na Mwandishi Wetu,Pwani
SERIKALI imeombwa kushirikiana na asasi za kiraia pamoja na makampuni ya kibiashara yaliyopo nchini katika kupiga vita vitendo vya rushwa na badala yake iache kusubiri msaada wa fedha kutoka kwa wafadhili.

Mkurugenzi wa asasi ya kitaifa ya Maendeleo ya Vijana (YPC) Israel Ilunde,alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza kwenye jukwaa la ufahamu wa kiraia lililofanyika Mjini Kibaha na kuwashirikisha wananchi pamoja na viongozi  mbalimbali.

Ilunde,alisema kuwa suala la rushwa bado ni changamoto kubwa hapa nchini japo limekuwa likipigwa vita kali na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli lakini pekee hatoweza bila kumpa ushirikiano.

Alisema kuwa,umefika wakati muafaka wa Serikali kukaa pamoja na makampuni ya kibiashara pamoja na asasi za kiraia ili kuweka misingi imara itakayosaidia kukomesha jambo hilo kuliko kusubiri watu wa nje waje kutusaidia.

Ilunde,alisema kupiga vita suala hilo linahitaji uzalendo wa wananchi wenyewe ambao watasimama katika kukemea vitendo vya rushwa na kwamba kusubiri fedha za wafadhili ni wazi kuwa hatutaweza kufikia malengo.

“Mimi nasema,tusiendelee kupokea fedha kutoka nje ili tupige vita rushwa lakini tunaweza kukomesha rushwa kwa kuwatumia wananchi wenyewe ambao ni wazalendo wa nchi  yao wanaoweza kusimama na kupiga filimbi juu ya janga hili,”alisema Ilunde.

Aidha ,Ilunde aliishauri Serikali kuhakikisha inatengeneza sheria ambayo itakuwa inawalinda watoa taarifa za rushwa ambapo hatua hiyo itawasaidia wananchi kuondoa hofu na hivyo  kutoa ushirikiano mzuri kwa Takukuru.

Hata hivyo,Ilunde alizitaka asasi za kiraia zilizopo nchini kuendelea kutoa elimu ya uraia kwa jamii ili waweze kufahamu madhara ya rushwa licha ya kuwa hawawezi kufanyakazi ya Takukuru lakini watasaidia kuelimisha jamii dhidi ya mapambano hayo







 





No comments